Mahakama ya Rufani yabatilisha adhabu ya kifo kwa aliyemuua mkewe

Arusha. Mahakama ya Rufani, imebatilisha na kuweka kando adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyekuwa amehukumiwa, Matho Joshua baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mkewe, Muse Sospeter.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubaini dosari ya kisheria wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ambapo Matho ambaye ni mpiga debe alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Septemba 23, 2022.

Dosari hiyo ni Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kutokufanya majumuisho kwa kuwaelekeza wazee wa baraza mambo muhimu ya kisheria yanayohusiana na kesi kabla ya kutoa maoni yao.

Kutoelekeza majukumu ya wazee wa baraza ni ukiukwaji wa kifungu cha 265 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Kutokana na sababu hiyo, majaji hao wamebatilisha na kuweka kando hukumu iliyopingwa na kuagiza jalada la kesi hiyo lirejeshwe Mahakama Kuu, kwa ajili ya kufanya majumuisho sahihi kwa wazee wa baraza ikiwa ni mujibu wa maagizo ya sheria.

Wakati huohuo imeagiza Matho abaki rumande ili kusubiri kuendelea kwa kesi na uamuzi kama ilivyoagizwa hapo juu.

Hukumu hiyo ya rufaa namba 643/2020 ilitolewa Agosti 9, 2024 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Stella Mugasha, Lameck Mlacha na Paul Ngwembe, walioketi Mwanza, ambayo imewekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kukubaliana na hoja moja ya rufaa ambayo ni dosari hiyo ya kisheria wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Matho alipandishwa kizimbani kwa kosa la kumuua mkewe, Juni 11, 2018 katika kijiji cha Isaba Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi watano ambao ni Magori Sospeter (dada wa marehemu), Fadhili Sospeter (kaka wa marehemu), Sumaku Rimbya, (mjomba wa marehemu), ofisa afya aliyeufanyia mwili uchunguzi na ofisa wa Polisi aliyemkamata na kumhoji Matho.

Muse (marehemu) awali alikuwa ameolewa na Mbarwa Mambya, lakini baadaye aliachika na kuolewa na Matho, walikuwa wakiishi wilayani Butiama.

Dada wa marehemu ambaye alikuwa shahidi wa kwanza, alidai siku ya tukio alipata taarifa mrufani alikuwa akimpiga dada yake (marehemu) na alipokwenda nyumbani kwao, alimkuta Matho anampiga marehemu kwa fimbo.

Alidai kumjulisha kaka yake (Fadhili) kisha akaondoka kuelekea kwenye mgodi wa dhahabu kwa shughuli zake za kibiashara, akiwa huko alijulishwa dada yake (marehemu) yuko nyumbani kwake lakini hali yake ni mbaya.

Alidai alilazimika kurudi na kumkuta marehemu akiwa na shida ya kupumua, akilalamika maumivu huku mikono na tumbo vikiwa vimevimba.

Kaka wa marehemu alidai alipokwenda nyumbani kwa dada yake alimkuta Matho anampiga mateke na fimbo na kuwa alipomsihi aache kumpiga na amruhusu ampeleke hospitali, hakukubaliwa.

Alidai Juni 16, 2018  hali ya dada yake ilizidi kuwa mbaya, hali iliyowalazimu wampeleke Hospitali ya Jeshi ya Kiabakari, ila kwa bahati mbaya alifariki dunia siku hiyo jioni.

Mwili wa marehemu kabla ya kuzikwa ulifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Butiama, ambapo ilithibitishwa kifo chake kilitokana na kuvuja damu nyingi ndani, huku mkono wa kushoto ukiwa umevunjika na bandama likiwa limepasuka.

Katika utetezi wake alioutoa chini ya kiapo, Matho alikana kuhusika na mauaji hayo na kukanusha ushahidi wa upande wa mashitaka unaomuhusisha kumuua mkewe na kudai Juni 8, 2018 mkewe alimuomba ruhusa anakwenda kwa wazazi wake na alimruhusu.

Alidai baada ya hapo alikwenda kwenye biashara yake ambapo anajishughulisha na upigaji debe kwenye stendi ya mabasi na gari alilokuwa akilipigia debe siku hiyo lilikuwa na dosari, ikabidi akalirekebishe.

Alidai aliporudi, alimkuta mkewe akinywa pombe na watu wengine, lakini alimpuuza na kuendelea na biashara yake, ila saa tisa alasiri Magori alifika na kumwambia kuwa mkewe alikuwa mgonjwa.

Matho alidai kumwagiza Magori kwenda kumpa uji mkewe, ila baadaye alijulishwa mkewe anataka supu hivyo aliandaa supu na kuwapa watoto wampelekee, na baadaye alipokwenda kumfuata mkewe alikataa kuondoka naye akimweleza anaumwa sana hivyo alimuacha.

Alidai siku iliyofuata alikwenda kumsalimia mkewe na kumkuta amekaa nje akiwa anakunywa pombe licha ya kudai kuumwa, kisha baadaye kukamatwa na kaka wa marehemu aliyekuwa na mtu mwingine, ambao walimfuata stendi, wakimtuhumu amemuua mkewe.

Jaji wa Mahakama hiyo akisaidiwa na wazee watatu wa baraza, walieleza kesi ya mashitaka ilithibitishwa bila kuacha shaka yoyote na kumuhukumu adhabu ya kifo.

Katika hati ya rufaa Matho alikuwa na sababu saba akiiomba Mahakama kufuta hukumu hiyo ya Mahakama Kuu na kutengua adhabu iliyotolewa dhidi yake.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Matho aliwakilishwa na Wakili Innocent Kisigiro, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Tawabu Yahya.

Wakili Innocent alidai Mahakama ya awali ilikosea kisheria kumtia hatiani Matho, kwani kesi haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka pamoja na Jaji kutokufanya majumuisho kwa kuwaelekeza wazee wa baraza mambo muhimu ya kisheria yanayohusiana na kesi kabla hawajatoa maoni yao.

Wakili Innocent alirejelea ukurasa wa 39 hadi 40 kwamba hoja muhimu za kisheria hazikuelekezwa kwa wazee hao wa baraza na kuiomba Mahakama kubatilisha mwenendo wa kesi hiyo.

Wakili huyo alieleza katika ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu haukuthibitisha kosa hilo, huku akipinga ushahidi wa kaka wa marehemu aliyeshindwa kuchukua hatua alipomkuta Matho anampiga marehemu.

Kwa upande wake Wakili Tawabu, alikiri majumuisho ya wazee wa baraza hayakufanyika vya kutosha na kutofanya hivyo kuliathiri shauri hilo na kwa maoni yake suluhu inayofaa ni kufuta hukumu, lakini mwenendo wa kesi ubaki kama ulivyo.

Jaji Ngwembe alisema ni msimamo wa kisheria kuwa kwa Jaji alipaswa kufanya majumuisho kwa kuwapa muhtasari sahihi ili kuwasaidia wazee wa baraza mambo muhimu ya kisheria yanayohusiana na kesi, kabla ya kuwahitaji kutoa maoni yao.

Jaji huyo amesema baada ya uhakiki wa kina wa kumbukumbu ya rufaa kama inavyoonekana katika ukurasa wa 39 na 40, hakuna ubishi kwamba Jaji wa Mahakama Kuu katika muhtasari wake kwa wazee wa baraza aliacha vitu muhimu iliwemo mazingira yanayounda kosa.

“Katika mazingira ya rufaa hii tunaona kwamba hakukuwa na muhtasari wa kutosha kwa kutoelekeza mambo muhimu ya kisheria kwa wazee wa baraza kwa nia ya kuwawezesha kutoa maoni yao kuhusu hatia ya mrufani,”alisema Jaji.

Jaji alieleza hivi karibuni Mahakama imeona pale ambapo kosa pekee la mahakama ya awali lilikuwa katika muhtasari usiofaa kwa wazee wa baraza, suluhu ni kupeleka jalada kwenye mahakama hiyo kwa ajili ya majumuisho sahihi kwa wazee hao.

“Mahakama imefuata mkondo huu katika kesi ya Silavio Kwapwela (supra). Ilitolewa hoja kwamba pale hali inaporuhusu, ni bora kuagiza muhtasari mpya na sahihi badala ya kubatilisha mwenendo mzima wa kesi,” alieleza Jaji.

Jaji Ngwembe alisema baada ya kuzingatia hilo, wanaona inafaa kufuata mbinu hiyo na kutumia suluhisho kama hilo katika rufaa hiyo, hivyo wameshindwa kukubali ombi la wakili Innocent la kubatilisha mwenendo mzima wa kesi.

“Tunafanya hivyo ili kubatilisha na kuweka kando hukumu iliyopingwa, muhtasari wote na matokeo ya maoni ya wazee wa baraza, tunaagiza  kuwa jalada la kesi hiyo lirejeshwe katika mahakama ya awali kwa ajili ya kufanya majumuisho sahihi kwa wazee wa baraza kwa mujibu wa maagizo ya sheria,” alihitimisha Jaji

Related Posts