Niko kwenye mgahawa mmoja hapa Shinyanga nangoja chakula cha jioni. Pembeni yangu wameketi watu wawili wanaoonekana kuwa karibu. Huenda ni mume na mke.
Nawaona kama watu waliokuja kwa mtoko wapate chochote kitu. Utaratibu mzuri kwa watu wanaopalilia mahusiano yao. Hata hivyo, tangu nimekaa hapa nusu saa iliyopita sijawasikia wakiongea. Hawaonekani kuwa na ugomvi, lakini pia hawaonekani kuwa na chochote cha kuongea.
Shukrani ziende kwa simu zao kubwa kubwa na za kisasa. Kila mmoja anaonekana kuwa na jambo la kufanya kwenye simu. Mwanamume mara kadhaa amepokea simu kwa vicheko.
Ukimsikia anavyoongea na simu utapenda. Bashasha. Uchangamfu. Mazungumzo yaliyojaa utani na mizaha inayoonyesha ukaribu na huyo anayezungumza naye. Mazungumzo ya simu yakiisha uso wa mwanamume huyu unabadilika.
Mwenzake, mwanamke, anamtazama kwa kuibia. Haonekani kuwa na ujasiri wa kumtazama machoni. Nahisi ni mila pengine. Kuna baadhi ya makabila kumtazama usoni mtu unayemheshimu ni kumkosea adabu. Hata hivyo, muda mwingi dada huyu alikuwa akitabasamu mwenyewe. Ingawa walikuwa pamoja na mwenzake kimwili, ufahamu wake na uzingativu wake ulikuwa kwenye vitu anavyokutana navyo mitandaoni.
Wenzi hawa wananikumbusha tabia zangu wakati fulani. Badala ya kuzungumza na kufurahia wakati mzuri nikiwa na watu ninaowapenda kama familia yangu, ningeweza kuwa ‘bize’ na wasiokuwepo hapo tulipo.
Kuna siku nilidondosha simu kioo chake kikaharibika. Sikuweza tena kujua anayenipigia na mahali pa kupokea. Sikuweza kusoma ujumbe unaoingia kwenye simu. Maisha yakawa magumu kweli siku hiyo.
Mwanangu wa miaka sita wakati huo alinionea huruma. Labda kwa kuona nilivyokuwa na simanzi alinitania kuwa angependa kuiombea simu ipone niweze kuitumia. Nikamuuliza kwa nini? “Baba umekosa kitu cha muhimu sana inachokihitaji. Simu ikiharibika kama hivi huwezi kuwa na amani.” Ujumbe mzito sana.
“Lakini baba kila ubaya una jema. Leo huna namna nyingine. Utakuwa na sisi kwa asilimia mia.” Kijembe kilinipata haswa. Kumbe watoto hawakuwa wanapenda tabia yangu ya kuwa nao lakini sipo. Inawezekana kufikisha ujumbe huo haikuwa rahisi, lakini mioyo yao ilikuwa na maumivu.
Huu ni upande wa pili wa teknolojia. Pamoja na kurahisisha maisha yetu, teknolojia imeathiri pakubwa namna tunavyohusiana. Kama ilivyo kwangu, ndivyo ilivyo kwa majirani hawa niliowaona hapa Shinyanga. Tunatumia teknolojia kuwasiliana na watu waliombali na sisi, lakini wakati huo huo inatutenganisha na watu tunaoishi nao.
Unaongea na walio nje ya nchi, maelfu ya kilomita mbali na upeo wa macho yako, saa nyingine, mkitazama nyuso mithili ya watu waliotenganishwa na kioo chembamba tu. Lakini unaoishi nao nyumba moja, wanaohitaji uwasikilize, useme nao, uzungumze nao, hamuwasiliani. Teknolojia ni kama inakuwezesha kuwasiliana na ulimwengu wote isipokuwa familia yako.
Hili la Shinyanga limenikumbusha maamuzi niliyoyafanya miaka kadhaa iliyopita. Nitajizuia kutumia simu ninapokuwa na mtu ninayezungumza naye. Simu ya mtu asiyekuwepo haiwezi kuwa muhimu kuliko mtu ninayezungumza naye.
Nilifanya maamuzi kuwa naweza kufuatilia simu na ujumbe nilioukosa wakati wa mazungumzo baada ya kumfanya huyo niliyenaye ajisikie kusikika, kueleweka na kuthamanika.
Niliweka ahadi kwamba nikishakubali kutoka na mtu ninajibika kumheshimu kwa kumpa muda wangu wote.
Nitaacha kushikashika simu. Nitamsikiliza. Kuliko nikacheke na simu nikiwa na mtu anayehitaji kusikilizwa na kueleweka, ni bora nimwambie ukweli kuwa huo sio muda mzuri wa kuonana naye. Kwenye enzi hizi za matumizi makubwa ya teknolojia, heshima ninayompa mtu inaendana na usikivu ninaoweza kumpa. Ukimheshimu utampa muda wako.