KWA mara nyingine tena Tanzania imetoka kapa katika Michezo ya Olimpiki 2024 wanariadha waliokuwa wamesalia katika michezo hiyo inayomalizika leo jijini Paris, Ufaransa Magdalena Shauri akimaliza wa 40, huku Jackline Sakilu akishindwa kabisa kumaliza mbio za marathoni, zilizoshuhudiwa Mholanzi mwenye asili ya Ethiopia, Sifan Hassan akivunja rekodi ya michezo hiyo akitumia muda wa 2:22:55.
Sifan alivunja rekodi iliyoweka na Muethiopia, Tiki Gelana aliyetumia muda wa 2:23:07 katika Michezo ya Olimpiki 2012 iliyofanyika London na kumfanya abebe medali ya dhahabu mbele ya Tigst Assefa wa Ethiopia aliyemaliza wa pili kwa 2:22:58 na Mkenya Hellen Obiri akimaliza wa tatu kwa muda wa 2:23:10.
Licha ya Magdalena kuanza vizuri mwanzoni mwa mbio hizo zilizoanza saa 3 asubuhi ya leo Jumapili, hali ilizidi kuwa mbaya kadri mbio zilizopokuwa zikisonga mbele kwa kuachwa nyuma na mwishoni kujikuta akiwa wa 40, wakati Jackline alijichomoa kabisa wakati mbio zikiwa kilomita 25.
Kuchemsha kwa wanariadha hao wa kike kumekuja saa 24 tu baada ya Alphonce Simbu kukwama kubeba medali ya kwanza ya Olimpiki kwa kumaliza wa 17 jana katika marathoni kwa wanaume pia, huku Gabriel Geay akijiondoa njiani na kuifanya Tanzania itoke tena kapa kama ilivyokuwa Olimpiki zilizopita za Tokyo.
Mbali na wanariadha hao waliokuwa wamebeba matumaini ya nchi, awali mcheza Judo, Andrew Thomas Mlugu na waogeleaji, Collins Saliboko na Sophia Latiff kuanza vibaya michezo hiyo inayofungwa rasmi leo usiku.
Mara ya mwisho kwa Tanzania kubeba medali za kwanza na pekee za Michezo ya Olimpili ilikuwa mwaka 1980 ilipofanyikia Moscow, Urusi kwa Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kunyakua medali za fedha kila mmoja.