Mbeya. Maadhimisho ya vijana duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Vijana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), huenda yakashindwa kufanyika kutokana na sintofahamu iliyojitokeza, ikiwamo baadhi ya makada wa chama hicho kukamatwa na Jeshi la Polisi.
Maadhimisho hayo ambayo hufanywa na Bavicha kila ifikapo Agosti 12, mwaka huu yalitarajia kufanyika viwanja vya Ruanda Nzove jijini Mbeya.
Katika hali isiyo ya kawaida sehemu iliyopangwa kufanyika tukio hilo la kitaifa, bado hakuna dalili za maandalizi huku askari wa Jeshi la Polisi wakiwa wametanda maeneo ya uwanja huo kuanzia asubuhi ya leo Jumapili, Agosti 11, 2024.
Jicho la Mwananchi limefika eneo hilo na kushuhudia gari aina ya Fuso lililokuwa limebeba matenti kwa ajili ya kujenga jukwaa likiwa limewekewa ulinzi wa askari Polisi, huku baadhi ya watu waliovalia nguo za Chadema wakifanya mazungumzo na Polisi hao.
Baada ya dakika kadhaa gari hilo liliondoka na mzigo wake uwanjani hapo, huku gari la Polisi likilisindikiza kwa nyuma.
Baadhi ya vijana wakiwa na bendera zao walikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi kilicho karibu na uwanja huo, baadaye kupandishwa kwenye gari la askari hao na kupelekwa uelekeo wa mjini.
Mapema akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya amesema maadhimisho hayo lazima yafanyike kutokana na kuwa ni tamaduni ya chama hicho.
Amesema pamoja na taarifa za baadhi ya vyama kupinga maandamano hayo, amesema Bavicha haijaandaa kitu hicho, bali wanachofanya ni maadhimisho ya vijana.
“Kile kilichoelezwa na baadhi ya vyama wanapinga maandamano, hatuwezi kutoa neno lolote kwa kuwa wako nje na kile sisi tunachofanya, Bavicha huwa tunaadhimisha kila mwaka, tulifanya hivyo Shinyanga mwaka jana tena Mwanza na kesho Jumatatu ni hapa Mbeya.”
“Maandalizi yapo hatua za mwisho kwani tunakagua uwanja kwa ajili ya kufunga jukwaa, viongozi na vijana wengine kutoka mikoa yote baadhi wamefika Mbeya wengine wako njiani hivyo tukio letu lipo vilevile,” amesema Chonya.
Chonya ameongeza katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi anatarajia kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe akiongozana na Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu.
“Watakuwapo pia wadau wa asasi mbalimbali za kiraia, wanaharakati, wanasheria na makundi mbalimbali ya vijana kwa lengo la kukutana kujadili mwelekeo wa chama,” amesema Mwenyekiti huyo.
Alipotafutwa baadaye kutokana na sintofahamu hiyo, simu zake za mkononi hazikupatikana hewani, huku taarifa zisizo rasmi zikieleza kuwa huenda naye ni miongoni mwa waliokamatwa.
Maeneo mbalimbali kumekuwapo na taarifa za magari yaliyowabeba vijana hao wa Bavicha yakizuiliwa kwenda jijini Mbeya.
Zuio hilo linafanyika ikiwa tayari Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekitumia barua Agosti 8, 2024, Chadema kukitaka kusitisha kongamano hilo ambalo linadaiwa linakwenda kuchochea uvunjifu wa sheria na amani.
Hata hivyo, Mnyika akizungumza na Mwananchi kuhusiana na barua hiyo alisema wameipokea na maandalizi ya kongamano hilo yanaendelea.
Kwa upande wake, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya leo Jumapili, Agosti 11, 2024, amepiga marufuku kufanyika kwa kongamano hilo, akionya watakaokaidi watachukuliwa hatua.
Ilichokisema Chadema, Bavicha
Saa 6:03 mchana wa leo Agosti 11, 2024, Katibu Mkuu wa Chadema, Mnyika kupitia akaunti yake ya X (zamani Twitter) ameweka ujumbe akisema: “Rais @SuluhuSamia ukiwa Amiri Jeshi Mkuu na IGP @tanpol sitisheni hatua haramu zinazofanywa na Jeshi la Polisi kuzuia shughuli halali inayofanywa na @bavicha_taifa ya maandalizi ya maadhimisho ya #SikuYaVijana#IWD2024. Zuiazuia na kamatakamata hii ni kinyume na haki na ni dharau kwa 4R mnazojinasibu nazo.”
Awali, akizungumza na Mwananchi Ofisa Habari wa Bavicha Taifa, Apolinary Boniface amedai miongoni mwa wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni Mwenyekiti wa baraza hilo Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya.
Amesema Chonya amekamatwa akiwa katika viwanja vya Ruanda Zove itakapofanyikia shughuli hiyo, pamoja na vijana wengine wawili wa baraza hilo.
Mbali na Chonya, Apolinary amedai mwingine aliyekamatwa ni Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Temeke, Deus Soka na msafara wake wa vijana waliokuwa katika gari aina ya Coasta kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kushiriki shughuli hiyo.
Kamatakamata hiyo, amesema imehusisha magari kadhaa likiwemo lililokuwa limebeba matenti kwa ajili ya shughuli hiyo, huku misafara ya vijana kutoka mikoa mbalimbali kwenda Mbeya nayo ikizuiwa.
Misafara iliyozuiwa kwa mujibu wa Apolinary ni vijana waliotoka Arusha, Moshi, Mara na Shinyanga wamezuiwa mkoani Iringa, huku waliotoka Zanzibar wakizuiwa Makambako Njombe na wale waliotoka Mwanza wamezuiwa Mtera.
Hata hivyo, amesema kamatakamata na zuia hiyo ya misafara haitakwaza shughuli hiyo kufanyika kwa kuwa, leo jioni anatarajiwa kupokelewa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu na wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya chama hicho.
“Hatuna lengo la kuahirisha maazimisho haya tunatarajia kuyafanya kama ilivyopangwa maandalizi yanaendelea,” amesema.
Undani zaidi wa kinachoendelea, fuatilia Mwananch