Polisi, Bavicha ‘ngoma bado Mbichi’ kongamano Mbeya

Dar/Mbeya. Magari 20 aina ya Coaster yaliyobeba vijana wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), yanadaiwa kuzuiliwa na Jeshi la Polisi kwenda mkoani Mbeya kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Hata hivyo, baraza hilo limeweka wazi kila kinachofanywa dhidi yao kuelekea siku hiyo, hakitakuwa kikwazo cha kuadhimishwa kwa siku ya vijana na maandalizi yanaendelea.

Bavicha ilitangaza kufanya maadhimisho hayo katika viwanja vya Ruanda Nzomve jijini Mbeya kesho Jumatatu, Agosti 12, 2024 na hata hivyo, shughuli hiyo imepingwa na Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mamlaka hizo za Serikali zimedai kuwa  maadhimisho hayo ya Bavicha yana viashiria vya uhamasishaji wa uvunjifu wa amani na vurugu katika shughuli hiyo, jambo linalokiuka matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Jeshi la Polisi nalo, katika taarifa yake limetoa marufuku ya kufanyika kwa shughuli hiyo, likiahidi liko imara kuhakikisha linadhibiti na kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka marufuku hiyo.

Katika kulitekeleza hilo, tayari misafara ya vijana kutoka mikoa mbalimbali kwenda jijini Mbeya imezuiwa, huku wengine hasa viongozi wa Bavicha wakiwa mikononi mwa jeshi hilo.

Wakati mamlaka zikifanya hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Moza Ally amewataka vijana wote ambao misafara yao inazuiwa na Polisi njiani, kuzima magari na kufunga barabara ili kuzuia shughuli yoyote isifanyike.

Amewataka wafanye hivyo hadi pale, jeshi hilo litakapoamua kuwaruhusu kuendelea na safari ya kwenda jijini Mbeya kuadhimisha siku yao Agosti 12, mwaka huu.

Ameambatanisha taarifa hiyo na onyo lake kwa Jeshi la Polisi kusitisha mara moja uamuzi wake wa kuzuia misafara hiyo ya vijana, akihoji kwa nini hawakuzuia shughuli ya vijana wa CCM iliyofanyika Zanzibar jana Jumamosi.

“Hapakuwa na shida yoyote, inakuwaje kama vijana wa Chadema tunataka kuadhimisha siku yetu ya vijana duniani mnaanza kutufanyia hujuma namna hii.”

“Hatuko tayari kuendelea kunyanyaswa, kuonewa katika nchi yetu, vijana ambao tayari wameshafika Mbeya ni Coaster 80, zilizozuiliwa ni 20 na zilizopo njiani ni 100,” amesema.

Kwa mujibu wa Moza, matarajio yao ni kuona Coaster 200 zilizobeba vijana zinafika Mbeya.

“Tupo tayari kwa namna yoyote ile kuadhimisha siku yetu ya vijana kama vijana wao walivyoadhimisha yao kule Zanzibar. Vijana wote mtakaozuiliwa kuendelea na safari, hakikisheni mnafunga barabara shughuli zozote zisiendelee mpaka mtakapoachiwa kuja jijini Mbeya,” amesema.

Amesisitiza maandalizi ya shughuli hiyo yanaendelea na wanatarajia kuwapokea viongozi mbalimbali akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu.

Marufuku ya Polisi, Msajili

Kutokana na vuguvugu hilo la Bavicha, Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano na mikusanyiko ya aina yoyote ile ya ndani au nje ya Mbeya, inayotaka kufanyika kwa mwamvuli wa kuadhimisha siku ya vijana duniani.

Sababu ya marufuku hiyo ni kile kilichoelezwa katika taarifa ya jeshi hilo kuwa, mikusanyiko hiyo inalenga kuleta uvunjifu wa amani Mbeya na maeneo mengine nchini.

Asubuhi ya leo Jumapili, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, Awadhi Juma Haji amezungumza na waandishi wa habari akiwa jijini Mbeya akipiga marufuku maandalizi na kutoa maagizo kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa (RPC).

Amesema tayari wamejipanga kikamilifu kukabilia na watu watakaothubutu kukiuka agizo hilo, huku likiwa limetoa maelekezo kwa makamanda wa Polisi nchi nzima kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto na kubaini watu waliojipanga kusafiri au kuanza safari kwenda Mbeya.

“Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kali na katazo kwa mtu au kikundi cha watu kinachojipanga kufanya mikusanyiko kuacha mara moja kwani limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi, usalama, amani na utulivu vinatawala nchini,” amesema.

Haji amesema wale waliosafiri kutoka mikoa mingine kwenda Mbeya kushiriki maadhimisho kama walivyohamasishwa wameshauriwa kusitisha safari hizo, kwani tayari wametoa maelekezo kwa makamanda wa Polisi nchi nzima.

“Nimetoa maelekezo kwa makamanda wa Polisi nchi nzima kufuatilia katika maeneo yao na wakibaini viashiria vya ambao wanafanya safari kuja Mbeya, kwenye kongamano lililopangwa kwa ajili ya uvunjifu wa amani kuwakamata na kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Haji amesema wamejipanga kukabiliana na viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani na kwamba halitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa mtu yoyote atakayekiuka katazo hilo.

Amesema kutokana na kauli zinazotamkwa na viongozi wa chama hicho ikiwamo, “kuamua hatma ya Taifa la Tanzania na kwamba wapo “Serious) sana kama vijana wa Kenya walijitambua na kuacha uteja na Serikali,” amenukuu.

Amesema mbali na nukuu hizo zipo taarifa nyingine ni viashiria tosha kuwa malengo yao sio kwenda kuadhimisha siku ya vijana duniani bali ni kuanzisha vurugu ili kusababisha uvunjifu wa amani.

Amefafanua kufuatia matamko mbalimbali ya viongozi Jeshi la Polisi limeamua kupiga marufuku maadhimisho na mikusanyiko ya aina yoyote ndani na nje, inayotumika kama mwamvuli katika siku hiyo duniani mkoani Mbeya na maeneo mengine.

Kauli zilizochukuliwa kuashiria uvunjifu wa amani kwa mujibu wa Haji ni “Kama kijana yeyote unaipenda nchi yako ya Tanzania, umeshalia miaka yako yote, siku hiyo ya Agosti 12, 2024 tunakwenda kuweka hatma ya Taifa letu la Tanzania mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote uliyepo popote Tanzania njoo uwanja wa Ruanda Nzomve Mbeya.”

Kauli nyingine ni, “Tupo serious sana na jambo hili, kwa hiyo vijana wote wa CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, siku ya tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuacha uteja kwa Serikali vijana wa Kitanzania na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.”

Kabla ya Jeshi la Polisi kutoa katazo hilo, tayari Msajili wa Vyama vya Siasa, alishaiandikia Chadema barua iliyosainiwa na Naibu Msajili, Sisty Nyahoza ya kuiasa isitishe shughuli hiyo kwa kile alichoeleza ndani ya barua hiyo kuwa, kuna ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Msingi wa hoja ya msajili ndani ya barua hiyo ni nukuu ya maneno yaliyozungumzwa na Katibu Mwenezi wa Bavicha, Twaha Mwaipaya, kama yanavyosomeka katika nukuu zilizotajwa na Jeshi la Polisi.

Walichoandika viongozi mtandaoni

Kabla ya tamko hilo la Bavicha, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani twitter), Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameandika akimtaka Rais Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura kusitisha kile alichokiita hatua haramu zinazofanywa nao kuzuia shughuli hiyo.

“Sitisheni hatua haramu zinazofanywa na Jeshi la Polisi kuzuia shughuli halali inayofanywa na Bavicha maandalizi ya maadhimisho Siku ya Vijana.

“Zuiazuia na kamatakamata hii ni kinyume na haki na ni dharau kwa 4R mnazojinasibu nazo,” aliandika.

Lissu naye katika mtandao huohuo, alionyesha kusikitishwa na kumwomba Rais Samia kulitaka Jeshi la Polisi kutotumia nguvu kuwazuia vijana kusherekea siku hiyo: “…siku ya Vijana Duniani inasherehekewa duniani kote. Kwa nini mapolisi wako wanazuia vijana wa Chadema barabarani & kuwakamata?”

Ujumbe mwingine uliochapishwa naye ni: “Kwa vijana wote mlioko na mnaoelekea Mbeya, Na mimi (Lissu) niko njiani kuja Mbeya kuungana nanyi.

“Kama ni kuzuiliwa au kukamatwa, na mimi wanizuie au kunikamata. Huu sio wakati kukaa kimya, kuogopa au kuuma uma maneno. Ni wakati wa kusimama na kuhesabiwa. Tupaze sauti kwa nguvu zetu zote,” ameandika.

Related Posts