KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Fredy Felix ‘Minziro’ amesema mechi tatu wanazocheza Uganda ni kipimo tosha cha wao kumkabili bingwa mtetezi Yanga kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Agosti 16 kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Kagera juzi ilijipima nguvu na Wahiso Giants na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yakifungwa na Cleophas Mkandala na Deogratias Mafie.
Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro alisema hawana hofu kuanza na Yanga msimu wanachoangalia ni namna gani wanajiandaa kwa kujiweka tayari wakicheza mechi za kimataifa za kirafiki nchini Uganda ambapo wameweka kambi.
“Tupo kambi Uganda mpango wangu ni kucheza mechi tatu za kirafiki kabla sijarudi na timu tayari kwaajili ya msimu mpya na mzunguko wa kwanza ni muhimu zaidi kuanza kuchanga karata zetu vizuri kwa kupata matokeo,” alisema beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Polisi Zanzibar na Yanga na kuongeza;
“Kukutana na Yanga mchezo wa kwanza hatuna hofu atatungeanza na timu tofauti bado tungecheza na hiyo timu hakuna hofu yoyote kikubwa ni kuandaa timu ya ushindani na kuhakikisha tunatumia vyema uwanja wa nyumbani.”
Minziro alisema anafurahia namna wachezaji wake wanavyopambana kujiweka tayari huku akiweka wazi kuwa anakikosi kizuri na anamatumaini makubwa ya kufanya vizuri msimu ujao.
“Nina wachezaji wazuri na wapambanaji nafura wanaonyesha uwezo mzuri kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi, nina kikosi kipana mechi na Wahiso Giants nimechezesha wachezaji naadhi na kesho ntacheza mchezo mwingine ili kuhakikisha kila mchezaji anapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake,” alisema Minziro.