Tabora. Ukistaajabu ya Mussa, utayaona na Firauni, ndivyo unavyoweza kusema baada ya waganga wa tiba asilia kutoka wilaya za Mkoa wa Tabora kueleza malalamiko yao kuhusu kutapeliwa na watu wanaojifanya askari Polisi.
Wamesema watu hao huwaweka chini ya ulinzi kwa tuhuma za kuwa na nyara za Serikali, kisha kuwataka kulipa fedha nyingi kama faini.
Katika kikao kilichofanyika leo Jumapili Agosti 11, 2024 mkoani Tabora, Shibula Maganga ambaye ni mganga wa tiba asilia kutoka Urambo, amesema ameshawahi kukamatwa na watu wanaojifanya Polisi. “Wakaniandikia faini ya Shilingi milioni moja, kwa kuwa sikuwashtukia, nilitafuta fedha hizo kwa shida na kulipa lakini baadaye nikagundua wale watu walikuwa ni matapeli,” amesema Maganga.
Ameiomba Serikali na viongozi waingilie kati suala hilo kwa kuwasaka watu hao wasiendelee na utapeli huo.
Mganga mwingine wa tiba asili, Kabula Rashid amesema baadhi ya vijana wanaojifanya ni askari, huwavamia na kuanza kuwabughudhi na wakati mwingine huwanyang’anya vifaa vyao wanavyofanyia kazi wakidai ni nyara za Serikali.
Amesema wanapojaribu kujitetea, huwataka wawalipe fedha nyingi ili wawachie vifaa vyao au la watawapeleka Polisi.
“Mimi nimeshawahi kukamatwa na kuambiwa nilipe faini ya milioni tatu kwa kuwa nimekutwa na mafuta ya kondoo bila kibali wakati sio nyara, na hawa vijana ukiwaambia wakupeleke mahakamani hawakubali, kwa hivyo tunaliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora lisimame kuhakikisha hawa watu wanakamatwa ili tufanye kazi zetu kwa uhuru tofauti na hali ilivyo sasa,” amesema Rashid.
Kwa upande wake, Chifu Nshoma Haiwa kutoka Ihama ya Usongo Igunga mkoani humo amesema waganga wote wa tiba asilia wako chini ya watemi wa mila na desturi, na malalamiko yao ya kukamatwa na kutapeliwa fedha yapo na tayari wameyafikisha kwenye ngazi husika.
“Malalamiko yao ya kukamatwa na kutapeliwa fedha na watu wanaojifanya Polisi ni kweli, maana kuna mganga mmoja aliwahi kukamatwa na kutozwa faini ya Shilingi milioni mbili na ushahidi upo, hili limekuwa tatizo kubwa kwa waganga wetu hivi sasa wanafanya kazi bila amani, tunawaomba Polisi wahakikishe hawa vishoka wanafanyiwa kazi ili waganga wetu wafanye kazi kwa uhuru tofauti na hali ilivyo sasa,” amesema Chifu.
Akizungumza katika mkutano huo, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Polisi Jamii mkoani humo, Raphael Mwandu amesema wameyapokea malalamiko hayo na wanayafanyia kazi.
“Askari wababaishaji kwa sasa hawana nafasi, wako wachache ambao hawana maadili tumekuwa tukiwabaini na kuwafukuza kazi, hatutakuwa tayari jeshi letu lichafuliwe na watu wanaojifanya askari,” amesema.
Hata hivyo, Mwandu amesema kuanzia sasa wataanza kuchukua hatua kali kuhakikisha waganga wanafanya kazi kwa utulivu.