Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amewapatia bima za afya watoto walemavu 600 waishio jijini hapa baada ya ofisi yake kupokea maombi ya uhitaji huo.
Mbali na bima, Gambo amewasaidia watoto na watu wazima wenye ulemavu vifaa saidizi ikiwamo miguu bandia 120, viti mwendo 600, fimbo 100, majiko 500 ya gesi, vyerehani vinane na vitanda 20 vyenye magodoro, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh400 milioni.
Akizungumza kwenye hafla iliyoandaliwa na Gambo ya kugawa vifaa hivyo leo Jumapili Agosti 11, 2024, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amepongeza jitihada hizo akisema changamoto kubwa kwa Serikali ni jinsi ya kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu.
“Msaada kutoka kwa watu binafsi kama alioutoa Gambo ni muhimu kwa kuwa asilimia kubwa ya watoto hawa hawawezi kumudu gharama za matibabu, lazima tuwashike mkono,” amesema Dk Mollel.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Gambo amesema vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na mashine za kushonea nguo, ni miongoni mwa maombi aliyopokea kutoka kwa wahitaji.
“Ofisi ya mbunge inapokea maombi ya mahitaji mengi na kwa kushirikiana na marafiki na wadau, tunaendelea kusaidia kadiri inavyowezekana,” amesema mbunge huyo.
Lakini ametoa wito kwa mashirika na wadau wengine kujitokeza kusaidia wahitaji katika jijini humo ili kutatua changamoto wanazokumbana nazo.
Amesema msaada ni moja ya ibada na kila mtu ana jukumu la kutoa sadaka kwa wahitaji, hivyo wasirudi nyuma.
Mmoja wa wadau waliochangia misaada hiyo, Atul Mittal amesema ameguswa kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu kutokana na sehemu ya faida waliyoipata katika uwekezaji wao walioufanya nchini.
Mwenyekiti wa wanawake wenye ualbino jijini Arusha, Anzirani Mohamed amesema misaada hiyo itasaidia kupunguza changamoto walizonazo na kuondoa utegemezi.