Tiketi ya Pamba kurejea Ligi Kuu iko Arusha

Pamba Jiji FC inakabiliwa na mechi mbili za Ligi ya Championship ugenini mkoani Arusha ambazo ni lazima kushinda zote ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Timu hiyo inashika nafasi ya pili kwa alama 61 tofauti ya alama tatu dhidi ya kinara Ken Gold FC yenye alama 64 inayohitaji alama mbili tu kupanda, tofauti ya alama mbili dhidi ya Biashara United na Mbeya Kwanza zinazoshika nafasi ya tatu na nne kwa 59.

Katika mechi 28 ilizocheza imeshinda 18 sare saba na kupoteza tatu huku ikifunga magoli 49 na kufungwa 16 ambapo inahitaji kushinda mechi zote mbili zilizosalia dhidi ya TMA Stars na Mbuni FC ili kupanda daraja moja kwa moja.

Kama Pamba Jiji itashinda mechi hizo itafikisha alama 67 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wake wa karibu Biashara na Mbeya Kwanza ambazo zikishinda mechi zao zote zitafikisha alama 65.

Endapo itashinda mchezo mmoja itafikisha alama 64 huku ikitegemea matokeo ya wapinzani wake, lakini kama itashinda moja na kutoka sare moja itafikisha alama 65 ambapo wapinzani wake wakishinda zote, mabao ya kufunga na kufungwa ndio yataamua timu ipi ipande na zipi zikacheze mtoano wa kupanda (play-offs).

Msimu uliopita mipango ya timu hiyo kupanda daraja moja kwa moja iliishia kanda ya kaskazini baada ya kutoka sare mechi mbili dhidi ya Mbuni FC na Africans Sports na kutoa nafasi kwa Kitayosce (sasa Tabora United), kuungana na JKT Tanzania kabla ya kufeli tena kupitia play-offs kwa kuondoshwa na Mashujaa FC.

Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji FC, Alhaji Majogoro ameiambia Mwanaspoti kwamba kama uongozi wanaendelea na maandalizi kuhakiksha wanakamilisha kile kinachotakiwa ili kushinda mechi hizo na kupanda daraja.

Amesema nguvu kubwa wamezielekeza katika mchezo wa Jumapili, Aprili 21 dhidi ya TMA Stars ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo mjini Karatu ambao kwao ni muhimu kushinda na kujitengenezea mazingira mazuri licha ya wapinzani wao kuendelea kuamini kama watapoteza.

“Katika mechi zilizobaki hakuna matokeo ambayo tunaweza kupata tofauti na ushindi kwetu, sisi pamoja na kwamba mpira una matokeo ya aina tatu lakini tunahitaji ushindi tu  kutimiza malengo,” amesema Majogoro.

Ameweka wazi kile kilichotokea msimu uliopita kwa mechi mbili za Kaskazini dhidi ya Mbuni FC na African Sports ambayo iliwavurugia mipango ya kupanda kwao ilikuwa ni kama funzo la namna gani inatakiwa kupambana katika mechi za mwisho.

“Ilikuwa ni kama funzo kwa sababu tuliona mechi moja inaweza kukuondoa kwenye reli ama kukufanya wewe upande daraja,” ameongeza.

Amefunguka kuwa hamasa ya mashabiki kutoka Mwanza kwenda Karatu kuipa sapoti timu hiyo siku ya Jumapili ni kubwa huku furaha yao kubwa ikiwa ni mechi hiyo kuchezwa kwenye uwanja ambao wote watakuwa ni kama wageni.

Timu hiyo inayoongozwa na kocha Mbwana Makata na msaidizi wake Renatus Shija wenye uzoefu na mashindano ya Championship, katika mechi zake tano za mwisho imeshinda nne na kutoka sare moja.

Mechi hizo ni dhidi ya FGA Talents (1-0), Polisi Tanzania (5-1), Ken Gold FC (2-2), Mbeya City (3-0), na Ruvu Shooting (3-1).

Related Posts