Kiongozi wa Dini Kenya asisitiza amani Tanzania kuelekea chaguzi

Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wakati Novemba mwaka huu ukitarajiwa kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani, viongozi wa kidini wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na hata baada ya chaguzi hizo.

Watanzania wakiliombea taifa Lao baada ya kuwasili katika viwanja vya makao makuu ya kanisa la New Life jijini Nairobi nchini Kenya

Wito wa amani kuelekea chaguzi hizo umetolewa leo Jumapili Agosti 11, 2024 na Kiongozi wa kanisa la New Life Prayer Centre and Church, Mchungaji Ezekiel Odera wakati wa maandamano ya hisani yaliyofanyika kanisani hapo.

Kilichochochea maandamano hayo ni kile alichoeleza, ni historia ya mataifa mengi kuingia katika machafuko baada ya chaguzi, hivyo asingependa kuona hilo linatokea kwa Tanzania pia.

Amesema amani ni nguzo muhimu kwa anayepigiwa kura, anayepiga kura na wale watakaoongozwa.

“Kwa mwaka jana nimefanya mikutano minne nchini Tanzania na miwili hapa kwetu Kenya. Na watu wengi wamekuwa wakiniuliza kwanini naipenda sana Tanzania na mimi nasema mahali alipo Mungu amani ipo na mwanadamu akijua alipo Mungu ni lazima atamfuata,” amesema.

Ameeleza ni furaha yake pia, kuona Watanzania wanakwenda kanisani humo kwa ajili ya kufanya maombi.

Mratibu wa kanisa hilo kwa upande wa Tanzania, Utukufu Peter amesema ni muhimu uchaguzi usiwe sababu ya kuvunjika kwa amani ya Tanzania ili ibaki na historia yake ya siku zote.

“Watanzania kutoka takribani mikoa yote tumesafiri kuja huku ili kufanya maombi haya pamoja na kiongozi mkuu wa kanisa letu, ambaye amekuwa karibu na taifa letu wakati wote, iwe shida au raha,” amesema.

Amesema ukaribu wa kiongozi wa kanisa hilo na Tanzania, ndiyo uliomsababisha wakati wa maporomoko ya matope Hanang achangie Sh milioni 100.

Related Posts