Seine-sational! Paris yatoa kwaheri ya ushindi kwa Olimpiki – DW – 12.08.2024

Cruise aliteremka kwenye waya mbele ya watazamaji 71,500, akashika bendera ya olimpiki na kurukia pikipiki, tukio lililowachangamsha wanariadha na mashabiki waliofurika katika uwanja wa Stade de France.

Katika dondoo ya kile ambacho ulimwengu unaweza kutarajia wakati Michezo hiyo itakapoelekea Los Angeles mnamo 2028, nyota huyo wa “Mission Impossible” kisha alionyeshwa akipanda ndege na kuruka angani hadi katika jiji la California kabla ya kupamba ishara ya Hollywood na pete za Olimpiki.

Kisha Bendi ya Los Angeles Red Hot Chili Peppers, mwimbaji Billie Eilish na rappers Snoop Dogg na Dr Dre wakatumbuiza tamasha ndogo kwenye ufuo ulioandaliwa na maji ya Bahari ya Pasifiki.

Soma pia: Olimpiki 2024: Marekani inaongoza jedwali la medali

Tamasha la ufungaji liliashiria mwanzo wa miaka minne ya maandalizi kuelekea Michezo ya Los Angeles, na mwanariadha wa Marekani Simone Biles alijiunga na meya wa Los Angeles Karen Bass wakati bendera ya Olimpiki ilipokabidhiwa rasmi.

Olimpiki Paris 2024 | Sherehe ya ufungaji| Tom Cruise
Nyota wa filamu wa Marekani Tom Cruise akiruka kutoka paa la uwanja wa Stade de France wakati wa sherehe ya kufunga michezo ya Olimpiki 2024.Picha: Phil Noble/REUTERS

Hapo awali, rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach alisema Michezo ya Paris imekuwa “michezo katika ubora wake”.

“Hii ilikuwa Michezo ya Olimpiki ya kuvutia kutoka mwanzo hadi mwisho,” Bach alisema. “Au nithubutu kusema: Michezo ya Seine-sational,” mkuu huyo wa IOC alizungumza kwa mzaha kuhusu mto huo unaokatiza jiji la Paris ambao ulikuwa eneo la sherehe ya ufunguzi.

“Wapendwa marafiki wa Ufaransa, mmependa Michezo ya Olimpiki. Na tumewapenda ninyi nyote,” Bach aliongeza.

Soma pia: Olimpiki Paris 2024: Wanariadha wa Afrika wang´ara

Takriban wanariadha 9,000 walikuwa wamefurika katika uwanja huo ili kuburudishwa na watumbuizaji na wasanii 270 katika hafla iliyotajwa kama usherehekeaji wa ubinadamu na nguvu ya umoja ya michezo.

“Tulijua mungen’ga, lakimi mmekuwa kivutio,” mkuu wa maandalizi ya Paris 2024 Tony Estanguet aliwaambia wanariadha. “Mmetufurahisha, mmetufanya tujisikie hai – ulimwengu uliuhitaji sana wakati huu.”

Marekani yaipiku China vita vya kuwania medali

Sherehe hiyo ilianza wakati shujaa wa kuogelea wa Ufaransa Leon Marchand — mshindi wa medali nne za dhahabu katika Michezo hii — alipochukuwa mwenge wa Olimpiki kutoka bustani ya Tuileries kuanza safari yake hadi uwanjani.

Paris 2024 - Sherehe ya ufungaji| Rais wa IOC Thomas Bach akipeperusha bendera ya olimpiki.
Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach akipeperusha bendera ya Olimpiki wakati wa sherehe ya ufungaji.Picha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Shujaa wa raga wa Ufaransa Antoine Dupont — ambaye aliongoza taifa mwenyeji kutwaa medali ya dhahabu ya raga ya wachezaji saba katika mojawapo ya vivutio vya mapema vya michezo hiyo — alibeba bendera ya Ufaransa hadi uwanjani huku wanariadha waliokuwa wakisherehekea wakimiminika uwanjani.

Sherehe hiyo ilifuatia siku 17 za michezo ambayo mara kwa mara ilikuwa na msisimuko, iliyofanyika kwenye maeneo ya kihistoria ya Paris, kuanzia Mnara wa Eiffel hadi Chateau de Versailles. Kinyume na sherehe ya ufunguzi iliyofanyika kwenye mvua, sherehe za Jumapili zilianza wakati jua la dhahabu lilipotua jiji kuu la Ufaransa.  

Soma pia: Paris yanga’a katika sherehe ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki

Siku ya mwisho ya michezo ilishuhudia Marekani ikiishinda China katika nafasi ya kwanza katika vita vya kuwania medali baada ya timu ya mpira wa kikapu ya wanawake ya Marekani kuishinda Ufaransa 67-66 na kutwaa dhahabu ya mwisho ya Michezo hiyo.

Ushindi huo — taji la nane mfululizo la mpira wa vikapu kwa wanawake la Olimpiki kwa Marekani — uliwahakikishia Wamarekani kumaliza wakiwa na idadi sawa ya medali za dhahabu na China, wakiwa na 40 kila mmoja.   

Marekani hata hivyo ilimaliza kileleni mwa jedwali la jumla la medali kwa jumla ya medali 126, huku China ikishika nafasi ya pili kwa 91.

Mholanzi awashangaza Waethiopia mbio ndefu

Jumapili ilianza kwa ushindi mnono wa mbio za marathon za wanawake na nyota wa mbio ndefu wa Uholanzi Sifan Hassan. Hassan alijitosa katika kile ambacho wengi walikichukulia kuwa kamari ya kichaa huko Paris, akishiriki katika mbio za mita 5,000, 10,000 na marathon.

Paris Olimpiki 2024| Marathon ya Wanawake| Shere ya ufungaji
Mshindi wa medali ya dhahabu ya mbio za marathon za wanawake Sifan Hassan, katikati, wa Uholanzi, akiwa na mshindi wa medali ya fedha Tigst Assefa wa Ethiopia, na mshindi wa medali ya shaba Hellen Obiri, wa Kenya kwenye jukwaa wakati wa sherehe za kufunga michezo ya Olimpiki 2024 kwenye Uwanja wa Stade de France, Jumapili, Agosti 11, 2024, mjini Saint-Denis, Ufaransa.Picha: Natacha Pisarenko/AP Photo

Lakini katika mbio za kukata na shoka, Hassan alimshinda Tigst Assefa wa Ethiopia na kutwaa dhahabu kwa sekunde tatu katika rekodi ya Olimpiki ya saa 2:22:55.     

Alianguka chini kwenye zulia la buluu mbele ya kuba la dhahabu la jumba la kumbukumbu la Invalides katikati mwa Paris kabla ya kukamata bendera ya Uholanzi kusherehekea mafanikio ya ajabu. Hassan alikabidhiwa nishani yake ya dhahabu katika hafla ya kufunga.

Related Posts