Mbeya. Serikali imeombwa kuweka mkazo kwa shule zote za sekondari nchini, zifundishe pia masomo ya ufundi na ujasiriamali, kwa lengo la kumuandaa mhitimu kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Imeelezwa kwa kufanya hivyo, kutasaidia kuondoa dhana ya wengi kuwa mtu anasoma ili aje kuajiriwa.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Aprili 27, 2024 na Mkuu wa Shule ya Sekondari Songwe Sunrise, Mpege Mwankotwa katika mahafali ya nane ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo.
Amesema mitalaa yote inapaswa kuendana na mabadiliko ya kidunia ya sayansi na teknolojia kwa watu kujengewa uwezo wa kujiajiri, badala ya kusubiri kuajiriwa.
“Ajira hazitoshi, vijana sasa wafundishwe ufundi na ujasiriamali mbali ya utaalamu anaosomea chuoni au mahala pengine popote.”
Amesema mwanafunzi akisoma ufundi au ujasiriamali na akawezeshwa mtaji, siyo rahisi kumkuta akizurura mitaani au kukaa vijiweni wanakokumbana na vishawishi lukuki vya uvunjifu wa amani.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wanaohitimu, Wiliam Mtandika amesema haikuwa kazi rahisi, lakini nidhamu na kujiamini waliyojengewa shuleni hapo, wanakwenda kuwa mabalozi wazuri huko waendako.
Mmoja ya wazazi na mdau wa elimu mkoani hapa, Ally Mwasala amewataka wanafunzi wanaohitimu kuendeleza nidhamu huku akisisitiza kuna maisha baada ya shule.
“Muda si mrefu mtaenda kwenye jamii zilizowalea, kama mtashindwa kujilinda kwa nidhamu hamtafikia malengo, tunatarajia elimu ya kidato cha sita mliyoipata iwe mfano huko nyumbani,” amesema Mwasala.