Agosti 16, 2024, Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kwa msimu wa 2024-2025 ikishirikisha timu 16 kuwania ubingwa unaoshikiliwa na Yanga.
Kabla ya kuanza kwa ligi, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho Soka Tanzania (TFF) ilikaa kikao Agosti Mosi, mwaka huu kujadili na kufanyia maamuzi maoni ya maboresho ya kanuni za ligi kwa ajili ya toleo la 2024.
Yamefanyika maboresho kadhaa katika kanuni za ligi miongoni mwa hayo ni ile ya 62 inayozungumzia wachezaji wa kigeni.
Palipofanyiwa maboresho ni katika ishu ya mchezaji wa kigeni anayesajiliwa ili usajili wake uweze kuthibitishwa na kuruhusiwa kucheza klabu inapaswa kumlipia Sh8 milioni. Awali kanuni hiyo ilikuwa mchezaji huyo analipiwa Sh4 milioni. Kumbuka wachezaji hao wa kigeni wanaozungumziwa hapa ni wale wanaosajiliwa katika kipindi cha usajili na siyo wale ambao wanaendelea kutumikia mikataba yao.
Kabla ya kwenda mbali, kanuni hiyo ya 62 kuhusu wachezaji wa kigeni, vipengele vyote vinasema hivi;
(1) Klabu ya Ligi Kuu inaruhusiwa kusajili wachezaji kumi na wawili (12) wa kigeni kutoka sehemu yoyote duniani (mazingatio kwa kanuni ya 62:4 ya kanuni hizi) na inaweza kuwachezesha/kuwatumia (kuwemo kwenye orodha ya wachezaji wa mchezo kwa siku husika) wachezaji wake wote kumi na wawili (12) wa kigeni katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu au Kombe la Shirikisho.
(2) Mchezaji wa kigeni atathibitishwa usajili wake baada ya TFF kuhakiki usahihi wa taarifa zake na kukamilika kwa taratibu za Uhamisho wa kimataifa na Mazingatio maalum kwa Utimizwaji wa Masharti ya Kisheria kwa wageni.
(3) Mchezaji wa kigeni wa ridhaa anayesajiliwa kwenye Ligi Kuu anaweza kuhamishwa kwa kufuata utaratibu wa uhamisho wa kimataifa kwa wachezaji wa ridhaa.
(4) Mchezaji wa kigeni anayeruhusiwa kusajiliwa kwenye Ligi Kuu ni yule anayecheza katika timu ya Taifa ya nchi yake au Ligi Kuu ya nchi husika. Mchezaji kutoka Amerika ya Kusini na Ulaya, lazima awe anacheza angalau kuanzia Ligi Daraja la Tatu (kitaifa, kutegemea mfumo kwa nchi husika). Mazingatio ya Daraja mchezaji analocheza kabla ya usajili wake kwenye Ligi ni kwa wakati husika au kipindi kisichozidi miezi sita tokea ameachana na timu yake ya mwisho kwa mchezaji aliye huru.
(5) Mchezaji yeyote wa kigeni anayesajiliwa katika Ligi Kuu atalipiwa ada maalum ya Sh8,000,000 (milioni nane) kwa msimu ili usajili wake uweze kuthibitishwa na kuruhusiwa kucheza.
Hicho kipengele cha tano ndicho kilichofanyiwa maboresho. Lakini vipengele vingine vimeendelea kubaki vilevile.
Ukiangalia hivi sasa ligi yetu imekuwa na wachezaji wengi wa kigeni huku zile zinazoshika nafasi tatu za juu kwa maana ya Yanga, Azam na Simba zenyewe kuelekea msimu wa 2024-2025 unaweza kusema tayari zimekamilisha usajili wake baada ya kila moja kufikisha wachezaji 12 kikanuni. Hivyo mastaa wapya kama Prince Dube, Jean Baleke, Joshua Mutale, Steven Mukwala, Jhonier Blanco, Mamadou Samake na wengineo watahusika TFF kuingiza si chini ya Sh600 milioni.
Ikiwa kila mchezaji mmoja wa kimataifa anayesajiliwa na timu ya ligi kuu anatakiwa kulipiwa Sh8 milioni, inatoa majibu ya moja kwa moja kwamba kama timu itasajili wachezaji 12 kikanuni inavyotakiwa, basi italazimika kulipa jumla ya Sh96 milioni.
TFF kupitia wachezaji hao kwa msimu wa 2024-2025 inatarajia kukusanya si chini ya Sh600 milioni kutoka timu shiriki ndani ya Ligi Kuu Bara, wastani ukiwa ni nyota watano kutoka kila timu. Ieleweke kwamba huo ni wastani haimaanishi kwamba kila timu ndiyo itakuwa na wachezaji idadi hiyo. Timu kama JKT Tanzania yenyewe haina mchezaji wa kimataifa.
Katika usajili wa dirisha kubwa unaotarajiwa kufungwa Agosti 15, 2024 siku moja kabla ya kuanza kwa ligi kuu, Simba imesajili wachezaji wapya 14 wakiwemo nane wa kimataifa.
Wachezaji hao nane wanaungana na wanne waliosajilia kutoka msimu uliopita kufikisha idadi ya wachezaji 12 wanaotakiwa kikanuni.
Nyota wapya wa kimataifa ndani ya kikosi cha Simba ni Moussa Camara, Valentine Nouma, Chamou Karaboue, Debora Fernandez Mavambo, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua na Steven Mukwala. Waliokuwepo tangu msimu uliopita ni Ayoub Lakred, Che Malone Fondoh, Fabrice Ngoma na Freddy Michael Koublan.
Wachezaji hao nane wa Simba, klabu hiyo inalazimika kulipa kiasi cha Sh64 milioni.
Kwa upande wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, wachezaji wapya wa kimataifa ni Chadrack Boka, Clatous Chama, Duke Abuya, Jean Baleke na Prince Dube, wanaungana na Djigui Diarra, Yao Kouassi, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Kennedy Musonda.
Yanga maingizo mapya wa kimataifa ni watano, hivyo wanalazimika kulipa Sh40 milioni kwa mastaa wao hao.
Franck Tiesse, Jhonier Blanco, Yoro Mamadou Diabby, Ever Meza, Mamadou Samake na Cheickna Diakite ndiyo mastaa wapya wa kimataifa ndani ya kikosi cha Azam, wanakwenda kuungana na Mohamed Mustafa aliyepewa mkataba rasmi baada ya awali kucheza kwa mkopo, wengine ni Yeison Fuentes, Yannick Bangala, James Akaminko, Gibril Sillah na Cheikh Sidibe.
Ukiachana na Simba, Yanga na Azam, timu zingine zitakazoshiriki Ligi Kuu Bara 2024-2025 ni Pamba na KenGold zilizopanda daraja. Pia zipo Mashujaa, Tanzania Prisons, Namungo, Fountain Gates, Singida Black Stars, Tabora United, JKT Tanzania, KMC, Coastal Union na Kagera Sugar.
Usajili bado unaendelea lakini mpaka sasa baadhi ya timu hizo zimeshusha vyuma vipya vya kimataifa ambavyo wanapaswa kuwalipa kila mmoja Sh8 milioni wathibitishwe kutumika ligi ikianza Agosti 16, 2024 ikiwa tayari ratiba imetolewa. Hizi hapa ni baadhi yao na mastaa wao wapya waliowaweka wazi.
Miongoni mwa nyota wao wapya wa kimataifa ni Samuel Antwi kutoka Ghana, Paulin Kasindi (DR Congo), Christopher Oruchum (Kenya), Mukeya Alain (DR Congo), Erick Okutu (Ghana) na Beny Nakibinde (Uganda). Nyota hao sita Pamba watatoa Sh48 milioni.
Erick Kapaito (Kenya), Moubarack Amza (Cameroon), Ritchi Nkoli (DR Congo), Erick Molongi (Angola), Djuma Shaban (DR Congo), Amade Momade (Msumbiji).
Joseph Guede (Ivory Coast), Tra Bi Tra (Ivory Coast), Ibrahim Imoro (Ghana), Mohamed Kamara (Sierra Leon), Koffi, Mohamed Damaro (Guinea), Emmanuel Keyekeh (Ghana), Arthur Bada (Ivory Coasta), Ande Cirrile (Ivory Coasta), John Nekadio (DR Congo).
Hernesi Malonga (Congo), John Makwata (Kenya), Banza Kalumba (DR Congo), Abdallah Hassan (Kenya), Anguti Luis (Uganda).