Matukio 10 Ngao ya Jamii 2024

FAINALI ya Ngao ya Jamii ilichezwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga imefanikiwa kuwa bingwa baada ya kuifunga Azam mabao 4-1.

Taji hilo ni la nane kwa Yanga katika Ngao ya Jamii tangu ilipoanzishwa michuano hiyo mwaka 2001, imezidiwa mawili na Simba ambayo inaongoza ikiwa nayo 10.

Msimu huu ni kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo tumeshuhudia Ngao ya Jamii ikishirikisha timu nne ambazo ni Yanga, Azam, Simba na Coastal Union. Msimu uliopita zilikuwa Simba, Yanga, Azam na Singida Fountain Gate.

Kumaliza kwa mechi za Ngao ya Jamii kunaashiria kwamba tunakwenda kuuanza msimu mpya wa 2024-2025 ambapo Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza Agosti 16, mwaka huu.

Hapa kuna mambo kumi yaliyojitokeza katika mechi hizo za Ngao ya Jamii kuanzia hatua ya nusu fainali, kusaka nafasi ya tatu na mchezo wa fainali.

Katika michezo ya Ngao ya Jamii tangu ilipoanza kuchezwa mwaka 2001, imeshuhudiwa mwaka 2024 kutokea kipigo kikubwa zaidi ndani ya dakika tisini wakati Azam ilipoichapa Coastal Union mabao 5-2 katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Kabla ya hapo, kipigo kikubwa kilikuwa cha mwaka 2002 ambapo Simba iliifunga Yanga 4-1, kisha 2019 Simba 4-2 Azam. Sambamba na fainali ya mwaka huu Yanga 4-1 Azam.

Dube, Fei Toto wamewaliza

Prince Dube amejiunga na Yanga msimu huu akitokea Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ huu ni msimu wake wa pili ndani ya Azam akitokea Yanga. Nyota hao wawili juzi wamewaliza mabosi wao wa zamani kwa kila mmoja kufunga bao.

Alianza Fei Toto kuwafunga Yanga dakika ya 13 likiwa ni bao la uongozi kwa Azam, mashabiki na viongozi wa Yanga walionekana kuingia ubaridi huku wale wa Azam wakilipuka kwa shangwe. Baadaye dakika ya 19, Dube akaisawazishia Yanga na kuwanyamazisha Azam. Safari hii mabosi wa Yanga na mashabiki wa timu hiyo wakajawa na furaha upande wa pili ikawa huzuni.

Kuanzia msimu uliopita wakati mechi za Ngao ya Jamii zimeanza kuchezwa kwa mfumo wa timu nne, Simba imeshiriki mara zote, lakini imekuwa na uhaba wa kufunga mabao ndani ya muda wa kawaida. Katika mechi nne ilizocheza ambazo ni sawa na dakika 360, imefunga bao moja tu kupitia Saleh Karabaka. Bao hilo limepatikana katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu mwaka huu waliposhinda 1-0 dhidi ya Coastal Union.

Kabla ya hapo, msimu uliopita nusu fainali ilitoka 0-0 dhidi ya Singida Fountain Gate, ikaja kushinda kwa penalti 4-2. Msimu huo ikacheza fainali dhidi ya Yanga, matokeo yakawa 0-0, wakashinda kwa penalti 3-1 na kuwa mabingwa. Msimu huu nusu fainali wamefungwa 1-0 na Yanga, wakaja kushinda 1-0 katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu dhidi ya Coastal Union.

Ukiangalia msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, zile nafasi nne za juu zilikuwa hivi; Yanga ambao ni mabingwa, Azam walishika nafasi ya pili wakifuatiwa na Simba, kisha Coastal Union nafasi ya nne.

Nafasi hizo walizoshika katika ligi, ndiyo zimejirudia katika Ngao ya Jamii msimu huu, Yanga wamekuwa mabingwa, Azam wakishika nafasi ya pili, Simba ya tatu na Coastal Union ya nne.

Unaweza kusema Feisal Salum ‘Fei Toto’ bado ana hasira na Yanga kwani hakuondoka vizuri ndani ya klabu hiyo. Katika kuonyesha hasira zake, amekuwa akipambana kila wanapokutana afunge. Jambo hilo amefanikiwa katika mechi mbili pekee kati ya tano alizocheza dhidi ya waajiri wake hao wa zamani.

Msimu uliopita walianza kukutana kwenye Ngao ya Jamii, Yanga ikashinda 2-0, baada ya hapo ikawa katika ligi, mechi ya kwanza Azam walichapwa 3-2, hakufunga, akaja kufunga waliposhinda 2-1, lakini pia akakwama kufunga katika muda wa kawaida walipocheza fainali ya Kombe la FA, akawaadhibu kipindi cha mikwaju ya penalti. Safari hii katika Ngao ya Jamii, amefanikiwa kufunga tena. Mara zote alizokutana na Yanga tangu aondoke klabuni hapo, timu yake ya Azam imeshinda mechi moja pekee na kupoteza nne. Katika kupoteza huko, Yanga imechukua ubingwa mara mbili mbele yake. Kombe la FA na Ngao ya Jamii.

Ni mara ya kwanza kushuhudiwa Ngao ya Jamii ikichezwa viwanja viwili tofauti. Tangu uanze mfumo huu wa kucheza timu nne kuanzia nusu fainali, msimu huu vimetumika viwanja viwili, New Amaan Complex uliopo Zanzibar na Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Ikumbukwe kwamba msimu uliopita mechi zote zilichezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Yanga yalipa kisasi cha 4-1

Ushindi wa mabao 4-1 ilioupata Yanga juzi ni kama kulipa kisasi baada ya mwaka 2002 kukutana na kipigo kama hicho kutoka kwa watani zao wa jadi, Simba.

Simba waliifunga Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwaka 2002 ikiwa ni msimu wa pili tangu kuanza kuchezwa mechi za mashindano hayo. Mwaka 2001 ambapo ndipo zilianza kuchezwa, Yanga iliifunga Simba mabao 2-1.

Unaweza kusema katika Ngao ya Jamii, Azam ni vibonde wa Yanga kwa sababu timu hizo zimekutana mara sita tangu mwaka 2013 ndani ya mashindano hayo, Yanga imeshinda mechi tano na Azam moja. Katika mechi hizo sita, tano ni za kuamua bingwa na moja ilikuwa nusu fainali.

Zile za kuamua bingwa matokeo yalikuwa hivi; Yanga 1-0 Azam (2013), Yanga 3-0 Azam (2014), Yanga 0-0 Azam (penalti 8-7 mwaka 2015), Azam 2-2 Yanga (penalti 4-1 mwaka 2016) na Yanga 4-1 Azam (2024). Ile ya nusu fainali ilikuwa mwaka 2023 matokeo yakiwa ni Yanga 2-0 Azam.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Coastal Union kushiriki Ngao ya Jamii, licha ya kwamba haikufanya vizuri ikimaliza nafasi ya nne, lakini imeshuhudiwa timu hiyo ikifunga mabao mengi kuizidi Simba.

Simba ambao walikuwepo tangu msimu uliopita ilipoanza kuchezwa Ngao ya Jamii kwa timu nne, imefunga bao moja katika jumla ya mechi nne, Coastal katika mechi mbili imefunga mabao mawili.

Katika mchezo wa fainali, ilishuhudiwa vikosi vya Azam na Yanga vikitawaliwa zaidi na wachezaji wa kigeni, huku wazawa wakiwa wachache.

Yanga katika kikosi chao kilichoanza cha wachezaji 11, wazawa walikuwa watatu pekee ambao ni Ibrahim Bacca, Dickson Job na Mudathir Yahya, upande wa Azam wazawa walikuwa watatu pia, Lusajo Mwaikenda, Adolf Mtasingwa na Feisal Salum.

Kikosi kizima cha Yanga kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Yao Kouassi, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Aziz Ki na Pacome Zouzoua.

Azam kikosi chao kilikuwa hivi; Mohamed Mustafa, Lusajo Mwaikenda, Cheikh Sidibe, Yeison Fuentes, Yannick Bangala, Yoro Diaby, Adolf Mtasingwa, James Akaminko, Jhonier Blanco, Feisal Salum na Gibril Sillah.

Ukiachana na mchezo wa fainali, pia ilishuhudiwa nusu fainali iliyowakutanisha Yanga na Simba, wageni walitawala kwa kiasi kikubwa, huku wazawa wakiendelea kujitafuta.

Simba iliyopoteza kwa bao 1-0, wazawa walioanza ni watatu; Shomari Kapombe, Mohamed Hussein na Edwin Balu. Yanga wazawa wao walianza wawili ambao ni Dickson Job na Ibrahim Bacca.

Kikosi cha Simba kilikuwa hivi; Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Che Malone Fondoh, Chamou Karaboue, Mzamiru Yassin, Edwin Balua, Debora Fernandes, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Joshua Mutale.

Yanga nao walianza hivi; Djigui Diarra, Yao Kouassi, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Prince Dube, Duke Abuya, Aziz Ki na Pacome Zouzoua.

Related Posts