Mzize: Chama ana jicho la pasi

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize amesema ubora wa pasi ya mwisho ya Clatous Chama ulimpa urahisi wa kukwamisha mpira nyavuni.

Mzize alifunga bao la nne na la mwisho kwenye ushindi wa mabao 4-1 ilioupata Yanga dhidi ya Azam katika fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. Mabao mengine yalifungwa na Prince Dube, Yoro Diaby (alijifunga) na Stephane Aziz Ki. Bao la Azam lilifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mzize alisema kabla ya kuingia uwanjani akitokea benchi, Kocha Miguel Gamondi alimtaka kuhakikisha anatumia nguvu zote kupeleka mashambulizi kwa wapinzani na ndicho alichokifanya.

“Alinionyesha mianya mingi ya kupita na kunisisitiza kutumia nguvu na akili kusogeza mashambulizi kwa wapinzani ndicho nilichokifanya, bao nililofunga nilianza kulitengeneza mwenyewe kwa kukokota mpita kutoka eneo la mbali la uwanja,” alisema na kuongeza;

“Baada ya kusogea karibu na boksi nilimpa pasi Chama ambaye ana jicho zuri la kutoa pasi za mwisho na kuwahi kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kupachika bao bila hiyana kiungo fundi wa pasi za mwisho alitoa pasi kwenye nafasi nzuri na mimi nilikwamisha mpira kambani.”

Mzize alisema Chama ni mchezaji ambaye anapiga pasi za akili na bora hivyo akiwa katika mazingira ambayo hakutarajia alikutana na mpira mguuni na kuukwamisha nyavuni.

“Chama ana jicho la kutoa pasi za mwisho na endapo kila mchezaji atacheza naye kwa usahihi basi atatulisha sana mipira ya mwisho na tutafunga sana, hili ni tela picha kamili linakuja,” alisema.

Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa mfungaji bora wa Kombe la FA msimu uliopita alisema baada ya kutwaa Ngao ya Jamii wanarudi kivingine Ligi Kuu Bara inayotarajia kuanza Agosti 16 mwaka huu.

Related Posts