Wahamiaji haramu wadakwa dereva atelekeza gari, atokomea

Arusha. Wakati wimbi la wahamiaji haramu likiendelea kutikisa nchini, wahamiaji saba raia wa Ethiopia na Somalia walioingia nchini kwa njia za panya, wamekamatwa wakiwa wamejificha kwenye shamba la mahindi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Agosti 12, 2024 na Jeshi la Uhamiaji mkoani Arusha kupitia kwa Ofisa Uhamiaji, Fakih Nyakunda amesema waliwakamata wahamiaji hao Agosti 8, 2024 saa mbili usiku.

Amesema watu hao walikamatwa eneo la Kisongo wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 801 AGJ.

Amesema walipata taarifa kutoka kwa raia wema ambapo waliweka mtego lakini na dereva wa gari hilo pamoja na watuhumiwa wengine walipobaini kuna mtego wa kuwakamata walikimbia na kulitelekeza gari.

“Baada ya kukimbia, watuhumiwa wanne walikutwa katika shamba la mahindi na wengine watatu tuliwakamata Agosti 9, 2024 saa nne asubuhi katika eneo la Duka Bovu ambapo mmoja kati yao ni raia kutoka Somalia,” amesema ofisa huyo.

Nyakunda amesema wanaendelea kulishikilia gari hilo na uchunguzi bado unaendelea ikiwa ni pamoja na kumtafuta dereva aliyekimbia na kutokomea kusikojulikana.

“Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria, tunaomba wananchi kutoa ushirikiano ili kukomesha biashara haramu ya usafirishaji wahamiaji haramu,” amesema Nyakunda.

Pia, ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha kwa namna yoyote ile na usafirishaji wa magendo wa binadamu,  na wote watakaobaini hatua zitaendelea kuchukuliwa ikiwamo kutaifisha magari wanayoyatumia kuwasafirishia kwa mujibu wa sheria.

Itakumbukwa kuwa hili si tukio la kwanza kutokea mkoani humo na ukanda wa kaskazini wenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga

Usiku wa kuamkia Julai 5 na 6, 2024, jeshi hilo pia liliwakamata wahamiaji haramu 31 kutoka Ethiopia baada ya lori la mzigo walilokuwa wanasafirishiwa kupata ajali baada ya kugongana na lori lingine, hivyo kulazimika kushuka na kujificha.

Watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Uwanja wa Ndege Kisongo uliopo nje ya mji wa Arusha.

Raia hao walidaiwa kuingia nchini wakitokea nchi jirani ya Kenya kwa lengo la kwenda Afrika Kusini.

Hivi karibuni Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na Mahakama ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, iliamuru kutaifishwa kwa magari mawili yaliyokamatwa yakisafirisha wahamiaji haramu 12 raia wa Ethiopia, likiwamo linalodaiwa kumilikiwa na mbunge.

Magari yaliyotaifishwa kwa amri ya mahakama hiyo ni Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 888 BTY ambalo jina la mmiliki linalosomeka kwenye nyaraka za umiliki, linafanana na la mbunge mmoja hapa nchini.

Gari lingine lililotaifishwa ni lori aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili KCV 571Y la nchi jirani, ambalo lilikamatwa katika mji wa Tarakea wilayani Rombo, Juni 19, 2024 likiwa na wahamiaji haramu watano.

Related Posts