Tuico yawaonya wafanyakazi kuibuka utitiri wa vyama vya wafanyakazi

Arusha. Chama cha Wafanyakazi, Tuico kimewataka wanachama wake kuwa  makini na utitiri wa vyama vinavyowatembelea na kuwashawishi kujiunga.

Amesema lengo la umakini huo  ni ili kuepuka kutapeliwa, kuibiwa au hata taarifa zao kutumika kwa manufaa ya watu binafsi.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 12, 2024 na Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka Tuico, Noel Nchimbi alipokuwa akitoa semina kwa wafanyakazi wa idara ya maji jiji la Arusha (AUWSA) juu ya masuala ya kazi, wajibu na haki zao kazini na kwa muajiri.

Nchimbi amesema hivi karibuni kumeibuka utitiri wa vyama vinavyojinasibu kutetea masilahi ya wafanyakazi wa kada mbalimbali, huku baadhi yao wakienda katika  ofisi za waajiri hasa za sekta binafsi na kuwashawishi wafanyakazi kujiunga navyo.

“Nitoe rai kwenu, pamoja na kuwa tumepewa uhuru wa kuchagua kujiunga na vyama, lakini tuwe makini nao wanapokuja kwanza asikuitie mkutano uchochoroni yaani nje ya ofisi unayofanyia kazi pia awe na kibali cha mwajiri, lakini jiridhishe na maswali kadhaa ikiwemo ofisi zao ziko ngapi na mikoa ipi, wana wanachama wangapi, lakini kubwa wana mikataba mingapi ya hali bora na piga simu mikoa husika aliyotaja uulize”.

“Lengo la kufanya hivi ni kuepuka utapeli, udanganyifu, wizi au matumizi ya taarifa zako utakazozijaza kujiunga kutumika vibaya na kukuharibia sifa baadaye, kwani kwa sasa kila kada au taaluma inajinasibu kuanzisha chama lakini nyingi ni kwa masilahi ya waanzilishi bila kuangalia wanachama wao” amesema Nchimbi.

Mbali na hilo, amewataka waajiri kuchuja sera za watu wanaojitokea kwenye ofisi zao kutaka kukutana na wafanyakazi wao kwa ajili ya kuwashawishi kujiunga na vyama hivyo.

Nchimbi amesema lengo la kutoa onyo hilo ni kwa sababu vilio vimekuwa vingi mitaani vya wafanyakazi kutapeliwa au kuibiwa fedha zao kwa madai ya kutoa kiingilio cha chama au dhamana ili kupewa mikopo, lakini haitekelezwi au inakuwa kandamizi.

Mwenyekiti wa wafanyakazi Auwsa, Said Galambo amesema semina hiyo iliyohusisha wafanyakazi wa idara ya maji walio wanachama na wasio wanachama wa Tuico imesaidia kupanua ufahamu wao juu ya usalama, haki na wajibu wao kazini na kwa muajiri.

“Hakuna haki bila wajibu, hivyo tumeona kadri unavyotekeleza wajibu wako ndivyo na haki itakavyopatikana hivyo tunaomba mafunzo kama haya yaje mara kwa mara ili wafanyakazi waendelee kuelewa na kutekeleza majukumu yao.”

“Pia waendelee kusaidia wenzetu waliorubuniwa kurudi kwenye vyama vya msingi,” amesema Said.

Naye Halima Mwahu ameiomba Tuico kuhakikisha wanaendelea kupigania mazingira ya mwanamke anapokuwa kazini kupata stahiki zake hasa kipindi akiwa mjamzito, uzazi hadi kunyonyesha.

“Waendelee kutupigania maana kuna baadhi ya maeneo unaogopa hata kubeba mimba maana unaiweka kibarua chako hatarini ikiwamo kufukuzwa, lakini tukijifungua tupewe muda wa kunyonyesha watoto kwa kupunguziwa saa za kuingia kazini,” amesema Halima.

Related Posts