Penzi la Fei na Yanga linakaribia mwisho wake

KAA katika televisheni yako halafu tazama namna penzi la waliloachana. Penzi la Fei Toto na Yanga linavyozidi kunoga. Wapenzi wawili wa zamani. Sasa hivi wanapitia katika kipindi kinachochekesha kidogo.

Jana Fei alifunga bao la kuongoza la Azam dhidi ya Yanga. Mbele ya kamera za Azam TV akakata mauno ya furaha. Kwa alichokifanya Fei alikuwa anawakera Yanga makusudi kabisa. Anajua kwamba hawampendi. Anajua kwamba hawajawahi kumsamehe tangu alipolazimisha uhamisho wake wa kutoka Yanga kwenda Azam.

Labda alikuwa ana haki ya kufanya hivyo. Aliwahi kuifunga Yanga katika pambano lake la kwanza akiwa na jezi ya Azam dhidi ya Azam lakini akaishia kuambulia kutukanwa. Baada ya hapo akaona hakukua na haja ya kuendeleza urafiki wake na Yanga. Mechi iliyofuata dhidi ya Yanga kule Zanzibar katika pambano la fainali za FA akafunga penalti yake na kuwanyamazisha Yanga kwa kuweka alama ya kidole mdomoni.

Bifu lake limeendelea juzi baada ya kufunga bao jingine dhidi ya Yanga. Linatuachia hadithi fulani hivi inayochekesha. Fei na Yanga kila mtu anamcheka mwenzake na kila mtu anajilaumu kwa kutokuwa na mwenzake. Fei anaikumbuka Yanga na Yanga inamkumbuka Fei. Mpaka sasa hakuna mshindi halisi baina ya bifu lao.

Tuanzie kwa namna ambavyo Yanga walitamani Fei haonekane hana lolote baada ya kuondoka kwao. Kwanza katika Ligi msimu uliopita Fei alikuwa anakimbizana na Aziz Ki mpaka siku ya mwisho ya kufungwa msimu. Bahati nzuri kwa Aziz akaibuka kuwa mfungaji bora.

Hata hivyo Fei alikuwa amejijengea heshima kwa watu ambao walikuwa wanasubiri kumshambulia kama akifeli kwa sababu pengine huu ulikuwa msimu wake bora zaidi pengine kuliko yote tangu alipoanza kucheza soka. Kuanzia Unguja hadi Dar es salaam. Kelele za kwamba Fei angepotea kwa kuondoka Jangwani zilikufa kifo cha mende.

Lakini hapo hapo Fei ameendeleza kuonyesha ukubwa wake kama Fei wakati Yanga wameendelea kumuonyesha ukubwa wao kama Yanga. Msimu uliopita walimalizia kwa ubingwa licha ya Azam kushinda pambano la mzunguko wa pili dhidi ya Yanga pale Temeke.

Tatizo kubwa ni kwamba Yanga wanamuonyesha Fei ukubwa wa klabu yao. Mataji. Walianzia pale ambapo Fei alikuwepo klabuni kwao. Walitwaa naye mataji mengi. Na baada ya kwenda Azam wameendelea kutwaa mataji mbele yake. Mwishoni mwa msimu uliopita walitwaa taji la FA mbele yake pale katika ardhi ya kwao Unguja.

Fei alifunga penalti yake kisha akawanyamizisha mashabiki wa Yanga kwa ishara ambayo imeendelea kuwakera mpaka sasa. Bahati mbaya mwisho wa mechi alinuna zake na hakwenda hata kupokea medali yake kwa sababu wenzake walimuangusha vibaya.

Juzi Yanga wametwaa ngao ya hisani pale Temeke mbele ya Azam. Fei alidhani kwamba labda pambano lile lingekuwa la kuwafunga midogo Yanga lakini haikuwezekana. Mwishowe kabisa Yanga waliondoka na kicheko kikubwa hadharani. Yeye alikuwa amefunga bao lakini Yanga walikuwa wameondoka na taji lao uwanjani.

Na sasa ni wazi kwamba Yanga wameendelea kumkumbuka kijana wao. Fei angekuwa staa zaidi ndani ya Yanga hii. Fei asingekosa namba ndani ya Yanga hii ambayo imeendelea kila kukicha. Hii inaendeleza hasira za Wanayanga kwa Fei. Hakuna kificho katika hili. Mtoto wao ambaye walimpenda na kumtunza. Mpaka leo hawajui nini kilitokea kwake akaamua kwenda upande ule.

Wakati huo huo Fei anaikumbuka sana Yanga. Hawezi kusema chochote hadharani lakini anajua kwamba angeendelea kuwa Yanga angekuwa ‘Mungu mdogo’ klabuni. Anajua kwamba msimu uliopita angeimbwa zaidi kuliko misimu yote aliyowahi kucheza  soka katika kiwango cha juu nchini. Bahati mbaya kwake ni kwamba msimu huo ulimkuta akiwa Azam. Sio Yanga wala Simba.

Haijulikani sana kwamba Azam wanamlipa kiasi gani Fei lakini ukweli ni kwamba Pesa sio kila kitu katika maisha yetu. Kuna furaha kutoka moyoni inakuwepo katika soka letu unapojikuta umeangukia katika hizi timu mbili za Kariakoo. Fei anakikosa kitu hivi kila anaposhika simu yake na kuangalia habari mbalimbali zinazohusu soka.

Nini kinafuata? Kabla ya kujadili nini kinatokea lazima tujadili uhalisi halisi. Ukweli ni kwamba hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kubadili ukweli kuhusu kitu kinachohusu Fei na Yanga. Na hii ndio raha ya mpira. Baada ya kila kitu kilichotokea Yanga haiwezi kumpenda Fei na wala Fei hawezi kuipenda Yanga.

Hata hivyo huu ndio utamu wa soka. Namna ambavyo mashabiki wa soka wanaweza kumchukia mchezaji wa timu yake au timu nyingine. Baada ya hapo mnabishana kuhusu maisha na mnajikuta yanaendelea. Hamna maamuzi makubwa kuhusu Binti Matata.

Fei anaionyesha Yanga ukubwa wake lakini na wao wanapambana kumuonesha Fei ulubwa wao. Mwisho wa siku  mwisho wa msimu huu utaamua vema kuhusu nank amejiandaa au vinginevyo.  Shukrani kwake baada ya kuonyesha ukubwa katika page yake.

Related Posts