Pemba. Makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa amesema nguvu kubwa ya chama hicho kuimarika na kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao ni vijana kuwa na misimamo imara isiyoyumbishwa.
Jussa ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 12, 2024 alipokuwa akizungumza na vijana, wanachama na wafuasi wa chama hicho Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya vijana duniani.
Amesema chama hicho kina mipango mizuri ya kuwatafutia fursa vijana kujiendeleza kiuchumi iwapo wataendelea kuwa wazalendo kwa chama hicho.
Amesema viongozi wa ACT Wazalendo wanafahamu changamoto za vijana kukosa ajira lakini kinaelekeza njia tofauti za mafanikio ikiwemo kwenye sekta binafsi.
“Niwaombeni vijana muendelee kukiunga mkono chama chetu, nguvu kubwa ya chama inategemea vijana ili tuweze kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu idara ya Mambo ya nje wa chama hicho, Nasra Nasor amesema miongoni mwa njia moja wapo ya kupata ushindi ni vijana kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kupiga kura.
Amesema kwa sasa ni muda kwa wasiokuwa vitambulisho vya Mzanzibari kuhakikisha wanavipata ili wawe na sifa ya kupiga kura.
Akizungumzia kuzinduliwa kwa programu ya ‘Binti Mzalendo’ amesema programu hiyo itawawezesha vijana wa kike kupaza sauti zao kupinga vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake na watoto.
Amesema kumekuwapo na vitendo vya udhalilishaji vinavyowakumba wanawake na watoto katika sekta mbalimbali, hivyo uanzishwaji wa programu hiyo itawawezesha katika mapambano ya vitendo hivyo.
Mapema, Makamu Mwenyekiti wa vijana Zanzibar, Naasor Marhuni amesema maadhimisho hayo yalikuwa na lengo la kuangalia na kujadili changamoto za vijana wanazokumbana nazo katika harakati zao za maisha.