Dar es Salaam. Washindi wa somo la hisabati mwaka 2024 Tanzania kwa ngazi ya kidato cha nne na sita, wamepata nafasi ya kushiriki mashindano yatakayohusha nchi zote za Afrika yanayotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini kuanzia Agosti 14, 2024.
Washindi hao wamepatikana kupitia mchakato uliofanywa na Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita) ambapo ilihusisha mikoa 12 na kufanikiwa kupata washindi sita, lakini watakaokwenda kuwakilisha nchi ni watano na mmoja aliyebaki kuonekana hana kigezo.
Wanafunzi hao ni Ambrose George Rutashobia kutoka Shule ya Sekondari ya Iyunga Technical, Ilham Abdulah Awadh kutoka Shule ya Sekondari Feza iliyopo Zanzibar, Mwanaarab Said Mbwana kutoka Shule ya Sekondari Lumumba iliyopo Zanzibar, Stella Ludan Maliti kutoka Shule ya Sekondari ya Marian na Zakaria Mataigi Mwita, kutoka Shule ya Sekondari Azania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 12, 2024, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania, Dk Said Sima ameishukuru Mamlaka ya Mawasilianp Tanzania (TCRA) kwa kuwalipia nauli ya kwenda na kurudi.
Mwenyekiti huyo amesema wanafunzi hao watasafiri Agosti 13, 2024 kwenda Afrika Kusini wakiwa na mwalimu mmoja na mashindano yataanza Agosti 14 hadi 20, mwaka huu katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, huku akitarajia ushindi kutoka kwa wanafunzi hao.
“Tumewandaa vya kutosha kuelekea kwenye mashindano, kwani tulikuwa na mfumo maalumu tuliowapa wanafunzi wetu kwa njia ya mtandao ili kujiweka sawa wakati wa mashindano na walikuwa wanafanya maswali ya hesabu, hivyo kupitia mazoezi yale nafikiri watashinda,” amesema Dk Said.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Hisabati kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Silvester Rugeinyamu anaiomba Serikali iwaunge mkono, kwani wanashindwa kushindanisha mikoa yote ya Tanzania kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha wa chama hicho.
“Watoto wanapaswa kupongezwa kwa jitihada zao, kwani hiki wanachokifanya sio kidogo, kupitia mashindano haya wanaweza kupata udhamini mkubwa na kusomeshwa nje ya Afrika,” amesema Silvester.
Chama cha Hisabati Tanzania kilianzishwa mwaka 1966, kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kimewapeleka wanafunzi mara kadhaa kwenye mashindano ya kimataifa ya somo la hisabati.
Miongoni mwa malengo ya mashindano hayo ni kuongeza motisha kwa wanafunzi kupenda somo la hisabati, kutambua vipaji mapema kwa wanafunzi na kuendelezwa na kujenga ushirikiano wa kitaaluma na diplomasia na mataifa mbalimbali duniani kwa wanafunzi na walimu.
Mashindano hayo hufanyika Agosti ya kila mwaka mwezi na washindi hutangazwa Siku ya Hisabati Duniani.