Dk Nchimbi amwagiza Waziri Masauni awaachie viongozi Chadema

Geita. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amemwagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo kuzungumza na waziri wake, Hamad Masauni, ili kuona namna ya kuwaachia viongozi wa Chadema waliokamatwa mkoani Mbeya, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Dk Nchimbi ameeleza hayo leo Jumatatu Agosti 12, 2024 alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Katoro iliyopo mkoani Geita anakoendelea na ziara yake akitokea mkoani Kagera.

Amesema alifanya jitihada za kuwatafuta viongozi wenzake wa vyama vingine vya siasa, ili wawe na mazungumzo kama vyama vya siasa, aliwasiliana na baadhi ya makatibu wakuu, hata hivyo alipata taarifa wengine wamekamatwa mkoani Mbeya.

“Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, ongea na Waziri, tunaomba muone uwezekano wa viongozi wa vyama vya siasa waliokamatwa kule Mbeya waachiwe huru.

“Mtupe nafasi na sisi wanasiasa tuzungumze, siyo mambo yote yanatatuliwa kisheria, mengine ni ya kisiasa,” amesema Dk Nchimbi akimwelekeza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani aliyeambatana naye kwenye ziara hiyo.

Viongozi wanaodaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi ni Mbowe, Katibu Mkuu John Mnyika, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), John Pambalu na viongozi wengine wa baraza hilo. Pia wamo viongozi wa Bavicha, Twaha Mwaipaya, Moza Ally, Deusdedith Soka na wengine.

Wengine wanaodaiwa kukamatwa ni Wakili Deogratias Mahinyila na waandishi wa habari wa Jambo Tv ambao ni Ramadhan Khamis na Fadhil Kirundwa.

Related Posts