Hatima dhamana ya kada wa Chadema aliyedaiwa kutekwa Agosti 22

Dar es Salaam. Hatima ya dhamana ya mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, aliyeripotiwa kupotea kabla ya Jeshi la Polisi Tanga, kutangaza kumshikilia siku 29 baadaye, na kisha kumfungulia kesi ya jinai, Kombo Mbwana sasa itajulikana Alhamisi Agosti 22,2024.

Mahakama ya Wilaya Tanga siku hiyo itatoa uamuzi wa pingamizi la dhamana lililowekwa na Jeshi la Polisi Tanga kupitia kiapo cha Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga (RCO).

Mahakama hiyo imepanga kutoa uamuzi huo ambao ama utamfanya Kombo awe huru kwa dhamana na kurejea uraiani au kuendelea kusota mahabusu, baada ya kukamilisha usikilizwaji wa pingamizi hilo la Jeshi la Polisi kuhusu dhamana ya mshtakiwa huyo.

Pingamizi hilo limesikilizwa leo Jumatatu, Agosti 12, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, anayesikiliza kesi hiyo, Moses Maroa, kuhusiana na zuio la dhamana yake lililowekwa na Polisi Mkoa wa Tanga.

Kombo anakabiliwa na kesi ya jinai mahakamani hapo inavyohusiana na matumizi ya kadi ya simu ya mkononi isiyosajiliwa. Alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 16, 2024, na kusomewa mashitaka hayo, ambayo hata hivyo aliyakana.

Mahakama ilisema dhamana yake ilikuwa wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa wanaishi pamoja na vitambulisho vya Taifa (Nida).

Alipelekwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini kwa kuwa ndugu zake hawakuwa na taarifa wakati anapandishwa kizimbani.

Julai 30, 2024 siku ambayo kesi hiyo ilitajwa, mawakili na ndugu zake walifika mahakamani hapo wakiwa wamejiandaa kukamilisha masharti ya dhamana wakitarajia kuondoka naye.

Hata hivyo, dhamana yake iliyeyuka baada ya RCO Tanga kuwasilisha mahakamani hapo kiapo cha kuzuia dhamana hiyo kwa maelezo bado wanaendelea na upelelezi, pia  wanatarajia kuwaongeza washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao wako katika maeneo mbalimbali nchini

Mawakili wa mshtakiwa huyo, Deogratius Mahinyila na Michael Rugina walipinga kiapo hicho wakidai kipo kinyume na utaratibu wa kisheria na RCO hana mamlaka hayo ya kuzuia dhamana, tena Mahakama ikiwa imeshatoa uamuzi wa masharti ya dhamana.

Hakimu Maroa aliamua kutengua amri ya masharti ya dhamana na akaahirisha kesi hiyo mpaka leo kwa ajili ya usikilizwaji wa kiapo hicho cha RCO.

Pia Hakimu Maroa aliutaka upande wa utetezi kuwasilisha kiapo kinzani kujibu kiapo hicho cha RCO kabla ya tarehe iliyopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa zuio hilo.

Kesi hiyo imesikilizwa chemba ambako waandishi wa habari na ndugu wengine wa mshtakiwa hawakuruhusiwa kuingia isipokuwa wazazi na mke wake.

Akitoa mrejesho kwa ndugu wa Kombo mmoja wa mawakili wake Michael Lugina amesema upande wa mashitaka umedai RCO amezuia dhamana kwa kuwa mshitakiwa anaweza kuingilia upelelezi unaoendelea.

“Sisi tumepinga kuwa dhamana ni haki ya mshtakiwa na mashitaka yanayomkabili yanadhaminika. Hivyo Mahakama imepanga kutoa uamuzi Agosti 22,” amesema Wakili Lugina.

Mwananchi lilipotaka kupata ufafanuzi kwa Hakimu Maroa ambaye  amejibu kupitia mmoja wa watumishi wa Mahakama hiyo kuwa hawezi kuzungumza na mtu yeyote anayemtaka amuone kesho Jumanne.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024, Kombo anakabiliwa na mashitaka matatu chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Katika shitaka la kwanza anadaiwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume na kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Anadaiwa kuwa Julai 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi wilayani na mkoani Tanga, alikutwa akimiliki laini (kadi ya simu) ya Tigo yenye namba (ICCID) 8925502042093621824, iliyosajiliwa kwa jina la Shukru Kahawa, na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.

Pia anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu, kushindwa kutoa maelezo ya mabadiliko ya laini hiyo iliyokuwa inamilikiwa na mtu mwingine.

Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Kijiji cha Kwamsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kupelekwa mahali ambako hata ndugu zake hawakupafahamu.

Julai 14, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard alitangaza kuwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma hizo, ndipo Julai 16 akapandishwa kizimbani.

Related Posts