Dodoma. Tanzania inatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wakulima wadogo unaolenga kuimarisha usalama na ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kuhakikisha usalama wa chakula unadelea kuwepo.
Mradi huo wa miaka mitano (2024-2028) unaofahamika kama Nourish utatekelezwa nchini kupitia Shirika la Maendeleo la SNV Netherlands kwa kushirikiana na Farm Africa, ukilenga kuimarisha usalama wa chakula kwa kaya za wakulima wadogo 168,000 katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Dodoma, Manyara na Singida.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 12,2024 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mradi huo, mkurugenzi msaidizi wa idara ya usalama wa chakula, Wizara ya Kilimo, Aradius Kategama amesema zipo changamoto mbalimbali zinazotishia usalama wa chakula, ikiwemo wakulima kutegemea mvua na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema ujio wa mradi huo utasaidia kuwafundisha wakulima kujifunza mbinu za kisasa za kilimo kuendana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kushika kasi.
“Mbinu ya kampeni ya kubadili tabia itakayofanywa na mradi wa Nourish kupitia wahudumu wa ngazi ya jamii na watu wenye ushawishi kutoa elimu kuhusu lishe katika kaya itasaidia kuinua lishe bora na afya njema.
“Pia uimarishaji wa uhusiano baina ya wakulima, waandaaji pamoja na masoko utapunguza hasara za mazao baada ya mavuno. Hii itasaidia uwepo wa chakula bora na wakulima kuwa na hakika kuwa mazao yatawafikia watumiaji,” amesema.
Kategama ametumia fursa hiyo kuiomba sekta binafsi kuwekeza kwenye uhifadhi, uchakatiji na masoko ya mazao, ili kuwasaidia wakulima wadogo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi, SNV Tanzania Michael Mcgrath amesema mradi huo utashirikisha watoa huduma za ugani, wazalishaji wa mbegu na wadau wengine muhimu, ili kuongeza maarifa na matumizi ya mbinu na teknolojia za kilimo zinazohimili mabadiliko ya tabianchi.
Amesema katika utekelezaji wa mradi huo, SNV na Farm Africa watafanya kazi kwa pamoja ili kushughulikia uzalishaji wa kilimo unaohimili mabadiliko ya tabianchi na kulenga lishe, kuongeza usambazaji wa chakula, upatikanaji wa chakula chenye lishe katika masoko ya ndani na kuboresha matumizi ya rasilimali za kaya, ili kuboresha usalama wa chakula na lishe.
“Hii inalingana na Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Tanzania (2022-2026) ambao unazingatia sekta ya kilimo kwa kuzingatia mabadiliko na ustahimilivu wa tabia nchi kupitia aina za mazao himilivu na kupunguza hasara baada ya mavuno,” amesema.
Takwimu zinaonyesha zaidi ya watoto milioni tatu walio chini ya miaka mitano wanakabiliwa na udumavu, hasa katika eneo la nyanda za juu kusini ambapo udumavu unafikia asilimia 46. 2.