ZAIDI YA VIJANA 70 KILA MWEZI WANAPATA HUDUMA YA MAFUNZO YA AFYA YA UZAZI MOROGORO

ZAIDI ya vijana 70 wanafika katika vituo vya afya mkoani Morogoro kila mwezi kwa ajili ya kupata huduma na mafunzo ya afya ya uzazi ikiwa baada ya watoa huduma kupata mafunzo kupitia Mradi wa Afya kwa Vijana uliofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti watoa huduma hao wamesema kuwa mafunzo hayo yameleta mwamko mkubwa kwa jamii kutokana na ongezeko hilo tofauti na hapo nyuma ambapo vijana 30 tu ndio walio fika katika vituo vya afya kupata huduma hizo.

Aidha, wamebainisha kuwa kumekuwa na changamoto ya wazazi kushindwa kufunguka kwa vijana wao kuhusu elimu hii ya uzazi na kutotaka wasielimishwe kutokana na dhana potofu kwamba itawafanya vijana wao wajiingize kwenye vitendo vya ngono.

Mtoa Huduma Ngazi ya Jamii (CHW) Rukia Mwamba katika Kijiji cha Fulwe Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alisema kutokana na wazazi kushindwa kuzungumza na Watoto wao kuhusu makuzi yao, kumekuwa na changamoto ya mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa kaswende na kisonono.

“Najisikia vizuri sana ninapopewa changamoto na kijana na kuitatua lakini tatizo kubwa ni watu kuwa na mtizamo hasi ambayo watu wanaamini kwamba vijana hawastahili kupata huduma hizi na wazazi pia kushindwa kuvunja ukimya na kuzungumza na watoto wao,” alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Uzazi, Baba, Mama na Mtoto wa Wilaya ya Morogoro Joyce Mganga alisema mradi huo umekuwa mkombozi kwa vijana na vituo vya afya kwa kuwa mbali na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya pia umeleta vifaa mbalimbali vya afya.

Muuguzi wa Afya katika Kituo cha Afya Fulwe Kata ya Mikese mkoani Morogoro Mwajuma Kassim, aliziomba mamlaka kuwahusisha wataalamu wa afya ya uzazi katika shughuli zao za kimila ambazo wanawafanyia watoto kama vile kuchezwa, kufundwa na ngoma za unyago ili watoe elimu ya afya ya uzazi.

“Huduma hii tulianza tangu mwaka 2022 kabla ya hapo vijana walikuwa wanakuja watatu kwa siku hivyo tukaamua kuweka muda wa ziada baada ya masaa ya kazi ili kuwapata vijana hawa, pia tumetenga siku za jumamosi ili kuwapa elimu hii na hiinimetusaidia kupata vijana wengi mpaka 200 kwa mwezi” alisema Mwajuma

Vijana wengi wanaofika zahanati ni vijana wa kike kulinganisha na wa kiume kutokana na wengi kutamani kukamilisha ndoto zao, hivyo basi wameona ni vyema kuweka nguvun katika kujifunza maswala ya uzazi wa mpango na afya ya uzazi kwa ujumla kabla hawajateleza na kupata mimba za utoto pamoja na magonjwa ya zinaa

Kwa upande wao watoto wa kiume wanakumbana na changamoto ya kushindwa kufanya maamuzi hasa matumizi ya kondom hivyo wanapofika kituoni wanafundishwa namna ya kutumia kinga hiyo kwa vitendo.


Related Posts