MAMLAKA ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa zaidi ya Sh 260 milioni kwa ajili ya maboresho na ukarabati wa jengo la usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kati ya kiasi hicho cha fedha, TPA imetoa Sh 251 milioni kugharamia ukarabati wa jengo la wagonjwa na Sh 10 milioni nyingine zilitumika kununua viti mwendo 20 na vifaa tiba vingine kwa ajili ya hospitali hiyo,
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Jumatatu wakati wa kupokea msaada huo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda aliishukuru TPA kwa msaada huo na kusema kuwa mamlaka hiyo ya usimamizi wa Bandari inajali sana jamii na kuziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo.
‘’Kipekee niipongeze Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam kwa kujitolea ukarabati wa jengo hili kwa ajili ya huduma ya usafishaji wa damu hapa hospitali ya Temeke.
“Ukarabati huu utasaidia sana kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji’’ alisema Mapunda kwa niaba ya Waziri Ummy.
Amesema kuwa Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza vya kutosha katika sekta ya afya hapa nchini, lakini pia bado inahitaji na kuthamini michango mbalimbali ya wadau wakiwemo TPA katika kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba.
Alisema kuwa uboreshaji wa huduma za afya ni moja ya vipaumbele vikubwa vya Rais Samia, hivyo kwa kiasi kikubwa TPA wanaunga mkono jitihada hizo.
“Tunawashukuru sana TPA katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia za kuboresha sekta ya afya hapa nchini inayogusa maisha ya watu.
“Uboreshaji wa sekta ya afya unasaidia watu kuwa na afya njema na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema.
Akitoa maelezo ya utendaji wa hospitali hiyo, Mapunda amesema kuwa uhitaji wa watu wanaohitaji huduma ni mkubwa ambapo kwa mwaka 2022/2023, hospitali ya Temeke ilihudumia wagonjwa 9,566 kwa watu waliokuwa na magonjwa yasiyoambukiza, ikilinganishwa na mwaka 2023/2024, ambapo wagonjwa 11,175 walihudumiwa, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 14.4.
Alisema kuwa vyanzo vya magonjwa hayo yasiyoambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa, ikiwemo matumizi ya chumvi na sukari kupita kiasi, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi.
‘’Katika kukabiliana na magonjwa hayo, amesema serikali imejipanga pamoja na mambo mengine, kuongeza kasi ya elimu na uhamasishaji wa jamii katika kuzuia na kudhibiti magonjwa hayo na kuijengea mazoea ya kufanya uchunguzi wa matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza na kufanya mazoezi.
Hata hivyo, Mapunda amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ina mpango wa kuziwezesha Hospitali zote za Rufaa za mikoa kutoa huduma ya kusafisha damu ili kutoa huduma kwa wananchi karibu zaidi na maeneo yao.
Akizungumzia juu ya msaada huo, Meneja wa Mizigo Mchanganyiko wa bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus alisema kuwa wameguswa na mahitaji hayo muhimu ya hospitali hiyo na kuamua kutoa kiasi hicho cha pesa katika kuunga mkono jitihada za Serikali.
“Mwaka jana mwezi Aprili, tulitoa msaada wa viti mwendo (wheelchairs) hopsitalini hapa, ndipo uongozi ulituomba msaada wa ujenzi wa jengo la usafishaji wa damu na sisi kama wadau bila kusita tukatoa kiasi hicho cha fedha ili kazi iendelee kama kauli mbiu ya Rais Samia inavyosema,” alisema.
Akizungumzia msaada huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk. Joseph Kimaro ameipongeza TPA kwa mchango wao ambao utagusa maisha ya watu wengi .
Dk. Kimaro alisema kuwa waliamua kujenga jengo hilo kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wagonjwa wa figo ambapo 2023 kulikuwa na wagonjwa 412, hivyo ikapelekea kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo hilo na sasa kwa jitihada za TPA limekamilika.