WAKATI Yanga ikionekana kufanya vizuri na kusalia kileleni hadi sasa, lakin beki wa kushoto wa timu hiyo, Joyce Lomalisa naye kibarua chake kipo hatarini.
Yanga iliyokuwa uwanjani jana jioni jijini Dar es Salaam kuvaana na Coastal Unioni ndio inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu (kabla ya jana) ikiwa na pointi 59, ikicheza mechi 23, ikishinda 19, sare mbili na kupoteza miwili.
Lomalisa, raia wa DR Congo alisaini mkataba wa miaka miwili ambao unaisha msimu huu, amekuwa na majeraha yanayomfanya kushindwa kucheza katika mechi muhimu na kutishia nafasi yake kikosini.
Aliumia katika mechi ya kimataifa dhidi ya Al Ahly ya Misri na dabi ya Yanga na Simba akitoka kipindi cha kwanza dakika ya saba, huku akiingia mbadala wake Nickson Kibabage.
Kwa upande wa rekodi msimu huu nako amekuwa hayuko vizuri, kwani hadi sasa ana asisti moja tu bila bao, huku mbadala wake Kibabage akiwa nazo nne.
Hii inazidi kuweka hatarini kibarua chake na kumpa nafasi Kibabage anayedaiwa alisajiliwa kwa mkopo wa miezi sita dirisha dogo akitokea Singida Fountain Gate ambako nako alichezea nusu msimu.
Kibabage anabebwa na vitu vingi kwa sasa ikiwemo umri kwani ana miaka 23 akiwa na rekodi ya kufanya vizuri toka timu aliyokuwa akiichezea kabla ya Yanga, huku akiwa bado ni kijana, kwa upande wa Lomalisa ambaye anaonekana kuchoka kutokana na kucheza kwa muda mrefu na umri ukiwa umesogea kwani sasa ana miaka 30.
Wapo wengine ambao vibarua vyao viliota nyasi msimu uliopita kutokana na changamoto kama hiyo, miongoni mwao ni Shaban Djuma Mkongomani mwenzake ambaye tangu amalizane na Yanga hana timu hadi sasa.
Hivi karibuni, Mwanaspoti liliweka bayana ripoti iliyowasilishwa mapema na Kocha Miguel Gamondi aliyetaka asajiliwe wachezaji wapya akiwamo beki wa pembeni wa kushoto, kiungo mkabaji kama au zaidi ya Khalidi Aucho na winga asilia anayejua kufunga mbali na mshambuliaji mkali kuliko waliopo sasa.
Hivyo kwa hali ilivyo kwa Lomalisa ni wazi kazini kwake kuna kazi, kwani atalazimika kufanya miujiza kwa muda uliosalia, japo anahusishwa na kwenda Afrika Kusini.