Dodoma. Jeshi la Polisi linamshikilia mlinzi wa Kanisa Katoliki Nzuguni jijini Dodoma kwa uchunguzi wa kifo cha msanii wa Bongo Fleva, Joseph Frank (46) maarufu Mandojo.
Mandojo alifariki dunia Jumapili Agosti 11, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakati akipatiwa matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Agosti 13, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo amesema saa 11 alfajiri ya Agosti 11, 2024 Mandojo alikutwa ndani ya uzio wa kanisa Katoliki Parokia ya Watakatifu Wote Nzuguni B jijini Dodoma.
“Akiwa amejificha ndani ya banda la mbwa… akiwa katika banda hilo mlinzi wa eneo hilo aitwaye Raphael Keneth (26) alisikia mbwa wakibweka kwa nje ya kibanda chao.
Na alipofika katika eneo hilo aligundua kuna mtu aliyejifungia ndani ya kibanda hicho,” amesema.
Amesema banda hilo lina vyumba viwili, hivyo Mandojo alikuwa amejifungia katika moja ya chumba katika banda hilo.
Amesema mlinzi huyo alianza kupamba na Mandojo kisha akaomba msaada kwa waumini waliokuwa wakifika katika kanisa hilo kwa ajili ya ibada ya kwanza asubuhi.
Kaimu Kamanda huyo amesema mlinzi huyo alifanikiwa kumdhibiti Mandojo kwa kushirikiana na waumini wengine na baadaye polisi walifika na kumchukua na kumpeleka hospitali.
“Jeshi la Polisi linamshilia Raphael Keneth kwa mahojiano. Uchunguzi wa tukio hili unaendelea na kwa sasa tunamshikilia huyo mmoja,”amesema.
Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Yohana Chacha mazishi ya Mandojo yatafanyika kesho Jumatano Wilaya ya Manyoni mkoani Singida baada ya kuagwa leo Ndachi jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Chacha, kaka yake hakurejea nyumbani kwa mkewe Nzuguni jijini Dodoma tangu alipoondoka Jumamosi Agosti 10, 2024, hali iliyowafanya ndugu kumtafuta.
Chacha amesema katika jitihada za kumtafuta walimkuta katika kituo kikuu cha polisi na aliwaomba wampeleke hospitali lakini alipopelekwa alifariki dunia muda mfupi akiwa katika idara ya wagonjwa wa dharura.