Polisi yaibua mapya sakata la Mbowe, wenzake

Mbeya. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema viongozi na wanachama wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakishikiliwa wameachiwa huru na kusafirishwa kwa ulinzi wa jeshi hilo hadi maeneo walikotoka wakiwamo wa jijini Dar es Salaam.

Jeshi hilo limesisitiza iwapo kuna mtu aliyekuwa ameshikiliwa na hajulikani alipo, familia zao ziulizwe kwa kuwa kila mmoja aliachiwa kwa utaratibu wake ikiwamo baadhi kuachiwa huru na wengine kwa dhamana.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Awadh Juma Haji, alipokuwa akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Agosti 13, 2024 kuhusu watuhumiwa waliowakamata kama wanaendelea kuwashikilia.

Viongozi na wafuasi wa Chadema, wapatao 520 akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho, John Pambalu na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu walitiwa nguvuni na jeshi hilo.

Mbali na hao, kamata kamata hiyo iliyofanyika mikoa mbalimbali nchini, iliwakumba waandishi wa habari, Ramadhan Hamis, Fadhili Kirundwa wa Jambo TV pamoja na Francis Simba ambaye ni mpigapicha wa Chanzo TV waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ofisi za kanda ya Nyasa, jijini Mbeya.

Kushikiliwa kwao kunatokana na uamuzi wa kuelekea jijini Mbeya kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilishaingilia kati shughuli hiyo na kupiga marufuku isifanyike kwa madai kuwa, ni vuguvugu la kuvunjwa kwa amani na vurugu ndani yake.

Baada ya kushikiliwa kwa saa kadhaa, usiku wa jana Jumatatu, Kamishna Haji alitangaza kuachiwa kwa baadhi na ambao hawakuachiwa ni wale walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana na kuwa na makosa zaidi ya moja ikiwamo jinai na kwamba jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.

Saa 3:52 asubuhi ya leo Jumatatu, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akitumia ukurasa wake wa kijamii wa X (zamani Twitter) aliandika: “Viongozi wakuu wa Chadema @freemanmbowetz@TunduALissu@jjmnyika@John_Pambalu wamerejeshwa Dar es Salaam na Polisi na wamejidhamini wenyewe! Kuna taarifa za baadhi ya viongozi wa Bavicha kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mbeya! Tutatoa taarifa baadaye!”

Kutokana na hilo, Mwananchi imezungumza na Kamishna Haji ambaye amesema waliokuwa wamekamatwa kwa kukaidi agizo la jeshi kuhusu kongamano la vijana, wote waliruhusiwa.

Amesema iwapo kuna yeyote ambaye hajulikani alipo, waulizwe familia zao kwa kuwa kila mmoja aliruhusiwa na kupewa eskoti ya polisi wakiwa huru na salama na kwamba hakuna aliyebaki kituo chochote cha polisi.

“Huyo anayesemwa hajulikani alipo aulize familia yake, wote waliokuwa wamekamatwa kama nilivyoeleza katika mkutano na waandishi wa habari, wameruhusiwa na kusindikizwa na polisi wakiwa salama,” amesema Haji.

Kamanda huyo amefafanua hadi sasa (ilikuwa saa tano asubuhi) hana taarifa zozote za kushikiliwa mtu yeyote kufuatia taratibu zote za dhamana kukamilika kwa waliokuwa na makosa zaidi ya moja kama ilivyoelezwa hapo awali.

“Waliokuwa na makosa zaidi ya moja wote walikamilisha taratibu za dhamana, hivyo hadi sasa sina taarifa za kukamatwa kwa mtu yeyote, kila mmoja aliachiwa kupelekwa kwake,” amesema kamishna huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya amesema waliokuwa wamekamatwa katika kituo walichokuwa wamewekwa makada takribani 54 ni mmoja pekee aliyeumizwa na kupelekwa kituo cha afya kwa matibabu.

“Sisi tulipelekwa kituo cha kati tukiwa viongozi kama wanne, mwenyekiti wa chama mkoa Masaka Caroli, katibu mkuu Gwamaka Mbugi, Hamad Mbeale na katibu mwenezi, Twaha Mwaipaya ambaye baadaye aliondoshwa kupekekwa sehemu nyingine,” amesema

“Hadi sasa sijapewa taarifa za jumla lakini kwa waliokuwa kituoni hapo, tupo salama na vifaa vyetu tumepewa isipokuwa mtu mmoja ndiye aliumizwa na kupelekwa hospitali,” amesema Chonya.

Chadema imetangaza kufanya mkutano na waandishi wa habari alasiri ya leo, makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taasisi mbalimbali

Related Posts