Geita. Aliyekuwa Ofisa Tabibu wa Kituo cha Afya Nyarugusu katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Paul Ng-wandu amekwepa kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja baada ya kulipa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh10,000.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne Agosti 13, 2024 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Samwel Maweda baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Katika shauri hilo namba 119 la mwaka 2023, ilidaiwa kuwa Dk Ng’wandu akiwa anatekeleza majukumu yake alijihusisha na vitendo vya rushwa na kujipatia Sh10,000 kutoka kwa mgonjwa.
Mwendesha Mashtaka na Wakili wa Serikali, Antidius Rutayuga akishirikiana na Ruth Ndetto ameieleza Mahakama kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a)(2)na (3)(a)(i)cha sheria ya kuzuia na kupambana cha mwaka 2022.
Akitoa hukumu hiyo, hakimu Maweda amemhukumu Dk Ng’wandu kulipa faini ya Sh500,000 kwa kila kosa au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja kwa makosa yote mawili aliyotenda.
Mshtakiwa amelipa faini na kukwepa kutumikia kifungo hicho cha mwaka mmoja jela.