Makambo aanza kutupia Ujerumani | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI kinda wa Tanzania anayekipiga FCA Darmstadt ya Ujerumani, Athuman Masumbuko Makambo ameanza kutupia baada ya kufunga bao moja waliposhinda 2-1 dhidi ya Viktoria Griesheim.

Hiyo ilikuwa katika mchezo wa Gruppenliga ya Ukanda wa Hesse nchini humo iliyoanza hivi karibuni.

Mechi hiyo ilipigwa Agosti 11, 2024 kwenye Uwanja wa RP1 Griesheim nchini Ujerumani ambapo Makambo alifunga bao la pili lililoipa timu yake ushindi wa pili tangu kuanza kwa ligi yao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Makambo alisema amefurahi kufunga bao kwenye mechi hiyo muhimu ya ligi licha ya kwamba alicheza kwa dakika 20 pekee.

“Natamani nifunge sana na naamini kwa nilivyojiandaa itakuwa hivyo, ili kocha aniamini na kunipa nafasi kubwa ya kucheza kama ilivyo kwa wengine nitapambana sana kuifungia timu yangu,” alisema Makambo.

FCA Darmstadt imecheza mechi mbili za ligi msimu huu na kushinda zote, imekusanya pointi sita ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya walio juu yake.

Related Posts