Sera hiyo ya kamata kamata inaungwa mkono katika mitandao ya kijamii na wanaharakati wanaouunga mkono utawala wa kijeshi, ambao wamekuwa wazi kabisa kuwakosoa watu wanaowaita “wakosa utaifa” kwa kuwapinga “wazalendo” waliowatiifu kwa utawala huo unaoongozwa na Kapteni Ibrahim Traore. Tangu Traore alipochukua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Septemba mwaka 2002, ukandamizaji umeongezeka hasa kwa wale wanaohoji kuhusu namna serikali hiyo ya kijeshi inavyowashughulikia wapiganaji walio na itikadi kali ambao Traore miezi michache iliyopita aliahidi kuwatokomeza.Kiongozi wa kijeshi Burkina Faso Ibrahim Traore asema uchaguzi “sio kipaumbele”
“Tumeshuhudia kuongezeka kwa ukandamizaji wa sauti huru au wakosoaji wa utawala huu wa kijeshi, na ukiukwaji wa haki za binaadamu,” alisema Ilaria Allegrozzi, mtafiti wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch katika ukanda wa Sahel. Jengine ni kwamba watu waliovalia nguo za raia, wanajitambulisha kama maafisa wa kijasusi na kuanza kuwakamata watu mjini Ouagadougou mchana kweupe. Visa hivyo pia vimeripotiwa katika maeneo mengine ya nchi. Siku wiki au hata miezi inapita wakati mwengine kabla ya jamaa zao kufahamishwa mahali wapendwa wao walipo.
Soma: Burkina Faso, Mali na Niger zakamilisha mpango wa ushirikiano wao
Mara nyengine waliotekwa au kupotea kwa muda hujitokeza na baadae wanachukuliwa na kufungwa rasmi jela. Wengine wanajitokeza wakiwa wamevalia nguo za kijeshi tayari kuingia katika uwanja wa vita kupambana na makundi ya wanamgaqmbo walio na itikadi kali. Allegrozzi anasema hii ni njia inayotumiwa na utawala wa kijeshi kuwanyamazisha wapinzani wake. Mtafiti huyo wa HRW amesema hatua inayochukuliwa dhidi ya wapinzani ni kinyume cha sheria na ni ukatili wa hali ya juu.
Utekaji nyara wa hivi karibuniulitokea wiki iliyopita lilihusu kinyang’anyiro cha rais mpya wa shirikisho la soka, Jeshi lilitaka kumueka mgombea wake katika nafasi hiyo. Wafuasi watatu wa mgombea Ali Guissou walitekwa nyara. Udhalimu haumuacho yeyote katika hili alisema Emmanuel Sawadogo ambaye ni mshirika wa Guissou aliyehoji visa hivyo vitatokea hadi lini? Mwezi mmoja kabla hilo kutokea waandishi habari wanne walipotea na kutojulikana waliko, waliripoti waandishi wasio na mipaka RSF waliosema wanaamini mkono wa utawala wa kijeshi umehusika katika hilo. Waandishi hao wanasemekana kutekwa kwa kuchunguza namna utawala huo ulivyonyamazia na kutotekeleza kikamilifu sera zake za uongozi
Kwa zaidi ya mwaka, utekaji nyara au kamata kamata imekuwa pia ikishuhudiwa miongoni mwa viongozi wa mashirika ya kiraia kwa mfano wakili mashuhuri nchini humo Guy Herve Kam aliyekamatwa mara tatu ndani ya miezi sita. Mfano mwengine ni baadhi ya maafisa wa serikali kama afisa mkuu wa zamani wa usalama Evrard Somda. Utawala wa kijeshi unawashutumu kwa kupanga njama ya kusambaratisha taasisi za taifa hilo.
Soma: Burkina Faso yawakamata Wafaransa wanne kwa ujasusi
Mambo kama haya yanayoendelea nchini humo yamewafanya raia wengi wa Burkina Faso kuitoroka nchi na kukimbilia katika mataifa jirani ili kuepuka madhila hayo. Hata hivyo bado mashirika ya kiraia yanaendelea kupaza sauti kupinga utekaji nyara wa watu nchini humo. Lakini Jumuiya ya kimataifa imekaa kimya. Hata katika bara la Afrika sauti ndani ya Umoja wa Afrika kukosoa kinachoendelea hazijasikika kikamilifu. Hata Kamisheni ya Umoja huo inayoshughulika na masuala ya haki za binaadamu pia imefumbia macho yale yanayoendelea Burkina Faso, alisema Allegrozzi.