Wanaume waongoza uchangiaji figo kwa asilimia 70

Dar es Salaam. Takwimu za uchangiaji figo nchini zinaonyesha kuwa wanaume wanaongoza kwa asilimia 70 ya uchangiaji ogani hiyo, huku wachangiaji wakiwa na umri kuanzia miaka 21.

 Hayo yamebainishwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakati hospitali hiyo ikiwa imeshafanya upandikizaji figo kwa wagonjwa 102, tangu ilipoanza kutoa huduma hiyo nchini mwaka 2017.

Akizungumza Agosti 13, 2024 katika maadhimisho ya siku ya uchangiaji wa viungo duniani, Mkuu wa Kitengo cha Figo katika MNH, Dk Jonathan Mngumi amesema takwimu za hospitali hiyo zinaonyesha jumla ya wachangiaji figo ni 102, wanaume wakiongoza kwa asilimia 70 kwa kujitolea kwa wazazi, watoto na ndugu zao.

“Wanaume wamekuwa wakijitolea viungo, hususani kwenye upandikizaji figo, japo wanawake nao wanajitolea lakini siyo wengi, tunawaambia upandikizaji ni salama hivyo wasiogope,” amesema Dk Mngumi.

Amesema kupandikiza figo si gharama kama ilivyo kwenye usafishaji damu (dialisisi) ambao unatakiwa kufanyika angalau mara tatu kwa wiki, wakati njia ya upandikizaji ni ya kudumu.

Mmoja wa wachangiaji figo, Juma Kanzaga (75) amesema hakuna sababu ya kumkataa ndugu kwa sababu amepata changamoto hiyo, kwani uchangiaji ni salama na hakuna shida figo inapotolewa.

“Kwangu imekuwa historia kubwa katika maisha yangu, ninawashukuru madaktari kwa kusaidia kuokoa maisha ya kijana wangu kwa njia salama ambayo itamfanya aishi miaka mingi zaidi.

Rehema Mungo mmoja wa watu waliopandikizwa figo amesema ni miaka mitano sasa tangu achangiwe figo na mtoto wake wa kiume akiwa na miaka 23 na hana changamoto yoyote.

“Namshukuru Mungu kwa kunipa mtoto mwenye huruma ambaye aliona thamani yangu na kukubali kutoa figo yake na sasa wote tupo salama, hivyo wengine wasiogope kufanya hivyo kwa familia zao,” amesema Rehema.

Hata hivyo, mpaka sasa Tanzania haina sheria ya upandikizaji wa viungo, ambao hujumuisha upandikizaji wa ini, moyo, mapafu, figo na utumbo mwembamba. Hivyo wachangiaji wa viungo kwa sasa nchini ni lazima wawe ndugu wa damu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Hispania la Upandikizaji Viungo (ONT), mwaka 2021 inakadiriwa viungo 144,302 vilipandikizwa.

Tangu kuanza upandikizaji wa figo mwaka 2017, Tanzania imekuwa ikitumia sheria ya kimataifa kwa kutumia viapo, vyeti vya kuzaliwa, uthibitisho wa ndugu, bodi ambayo inakubali upandikizaji husika, lakini pia kumekuwa na mratibu wa upandikizaji.

Katika uzinduzi wa jengo la Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma Februari 2023, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema wapo katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria kuruhusu watu kuchangia viungo vya ndani ikiwamo figo.

“Lakini sisi hatuna sheria ya kuchangia viungo vya ndani ndiyo tunataka kuitunga kwa hiyo tunahitaji kutoa elimu, unaweza kutoa figo yako moja na ukaishi vizuri tu,” alisema Ummy.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi pasipo kutaja kiasi amesema wamepokea fedha kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya upandikizaji figo na tayari wamepandikiza watu 12.

“Naomba kutoa rai kwa wale wote ambao hawana fedha kamili za kupandikizwa leo kwa kutumia siku hii ya upandikizaji duniani, Muhimbili inatoa ofa kwa wagonjwa wengine 10 ambao wanataka kupandikizwa figo,” amesema.

Amesema wahitaji wafike kujiandikisha kwa Dk Mngumi na watapatiwa huduma kutokana na fedha za Rais Samia, hivyo wasitoe visingizio.

Profesa Janabi amesema la muhimu kwa wachangiaji wajitokeze, kwani hawatumii zaidi ya saa 48 kama kila kitu kikiwa sawa.

Amesema kwa sasa upandikizaji unaofanyika ni kwa ndugu na unafuata taratibu zote za uchangiaji wakisubiri Serikali kutoa mwongozo kuhusu watu wengine kujitolea viungo.

Amesema kutumika kwa utaratibu huo ni kwa ajili ya kuzuia watu wenye kipato cha chini kugeuza figo zao biashara, bila wao kupenda ilimradi wapate fedha.

Tafiti zinaonyesha watu 430 waliochangia figo wanaishi maisha marefu na hakuna athari zozote zilizotokea baada ya hatua hiyo, pia hakuna tofauti na wale ambao hawachangii figo.

Amesema kusafishwa figo kwa baadhi ya wagonjwa wanaofika hospitali ni daraja wakati wakisubiri upandikizwaji wa figo na utaratibu wake, husafishwa mara tatu au mbili kwa wiki. Amesema huduma hiyo ina gharama kubwa.

Profesa Janabi amesema, “Serikali peke yake haiwezi kugharamia, kwani Muhimbili tuna awamu tatu asubuhi, mchana na jioni ambazo wagonjwa wanakuwa 190 na wanatakiwa kutumia vitu ambavyo vinagharimu Dola 70 hadi 100 za Marekani ambazo ni gharama kubwa.”

Akijibu ombi la matumizi ya bima ya afya katika upandikizaji, Profesa Janabi amesema wanaotumia bima watalazwa katika wodi binafsi ambayo ni namba 17, hivyo wawe huru kwenye matumizi ya bima zao.

Related Posts