Unguja. Ili kuwawezesha wananchi kiuchumi, Serikali imetenga Sh39.5 bilioni zitakazotolewa kwa mkopo usiokuwa na riba, hususani kwa wanawake na vijana Zanzibar.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Agosti 13, 2024 wakati wa kufungua mafunzo ya kutengeneza umeme jua katika kituo cha kuwafunza wanawake kutengeneza vifaa vya umeme wa jua na ujasiriamali (Barefoot College) Kinyasini Mkoa wa Kaskazini, Unguja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wanananchi Kiuchumi (ZEEA), Dk Juma Burhan Muhamed amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 wametengewa Sh39.5 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa wananchi, hususani wanawake na vijana.
Amesema pia wametengeneza mifumo ya kuwawezesha wananchi, ukiwemo wa ZEEA Masoko unaounganishwa na Shirika la Posta utakaowasaidia wajasiriamali kusafirisha bidhaa zao kimtandao bila kutumia gharama.
“Huu ni mfumo ambao mjasiriamali anaunganishwa na atasafirisha bidhaa zake nje ya nchi bila kutumia gharama, kwa hiyo haya ni maono ya Serikali ambayo inataka wajasirimali hususani wanawake kujikwamua kimaisha,” amesema.
Amesema wameshatoa mikopo kwa vikundi 753 vya ufugaji nyuki na tayari wakala imeshapata Sh96.7 milioni kutoka vikundi 53 vya ufugaji nyuki.
Msimamizi wa kituo hicho, Brenda Ndossi amesema mwanzo walikuwa wanachukuliwa wanawake wanakwenda nchini India kwa miezi sita kupewa mafunzo hayo, mwezi mmoja ni kujifunza lugha kwani walikuwa wanakutana na zaidi ya nchi 80 duniani.
Amesema baada ya kurudi walikuwa wanarudi vijijini kwao wakiwa na vifaa kwa ajili ya kuweka umeme katika vijiji ambavyo havina nishati hiyo, ndiyo baadaye ikaonekana kituo hicho kifunguliwe Zanzibar kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumefanya miradi tofauti, ikiwemo utengenezaji vifaa vya umeme jua, ushonaji na ufugaji nyuki na masharti ya mwanamke kujiunga lazima awe na umri wa miaka kuanzia 35 hadi 55 ambaye hawezi kuhama kwenye kijiji chake, awe kwenye ndoa au hayupo.
“Pia ni wanawake ambao hawakwenda shule, kwa hiyo wanataka kuwainua katika uchumi wao na Taifa kwa ujumla. Kazi kubwa inayofanywa na wanawake hao ni kuunganisha vifaa vya umeme jua na vikiharibika namna ya kuvifanyia matengenezo,” amesema.
Msajili wa asasi za kiraia, Ahmed Ahmed amesema taaluma hiyo inakwenda kusaidia katika maisha yao na kunyanyua uchumi wa kinamama.
Baadhi ya wanawake wameeleza namna walivyofarijika kujiunga na mafunzo hayo na jinsi walivyokuwa na hofu awali.
Tabia Khamis Mzaga, aliyejifunza ufundi umeme jua amesema, “mwanzoni nilikuwa napata wasiwasi kabla sijajiunga, lakini baadaye nikazoea na kwa sasa nafurahi nimejifunza kutengenza vifaa vya umeme na nikimaliza naenda kijijini kwangu kuisaidia jamii.”
Kazija Gharib Issa, aliyepata mafunzo hayo na kwa sasa ni mkufunzi katika chuo hicho amesema amenufaika, akieleza amejenga nyumba na anawasomesha watoto wake kipitia ufundi huo.
Hata hivyo, amesema haikuwa kazi rahisi kwani mwanzoni alipata changamoto ya mitazamo ya kijamii kuonekana kwamba mwanamke hawezi au hastahili kufanya kazi hizo, lakini hakujali badala yake aliangalia anachokitaka.
Amesema kuna wakati hukabiliwa na changamoto ya baadhi yao kukataliwa na wanaume wao kujiunga katika mafunzo hayo.
Mjasirimali, Salma Mzee Mussa amesema baada ya kumaliza mafunzo anatamani kuwa fundi mkubwa wa kutengeneza vifaa vya umeme wa jua, ili kuisaidia jamii na kujikwamua kiuchumi.
Amesema, “namshukuru mume wangu aliniruhusu na watoto wangu kila Jumapili wanakuja kunitembelea. Ninatamani nikimaliza mafunzo niende kuwasaidia wanakijiji kuwaunganishia umeme.”
Awali, akifungua mafunzo hayo, Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said ameeleza kuvutiwa na mradi huo akisema utasadia na kuleta matokeo mazuri kwenye jamii.
Amewataka wasimamizi wa kituo hicho waanze kuainisha wanawake wanaomaliza mafunzo hayo wanavyokwenda kunufaisha jamii kwenye vijiji vyao.
“Mpango huu ni mzuri hapa tumeona wanawake mainjinia, wanaotengeneza umeme, inafurahisha,” amesema.
Amesema mpango huo unasaidia jitihada za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini na kuchochea harakati za kiuchumi.