Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), inatarajia kuanzisha huduma ya ‘Ride Sharing’ kabla ya kuisha mwaka huu wa fedha 2024/25.
Watu tisa hadi 14 wataweza kupanda gari moja kwa kuomba kupitia mitandao ya simu hata kama wapo vituo tofauti.
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumanne, Agosti 13, 2024 Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Latra, Johansen Kahatano amesema wameamua kuja na huduma ili kuendelea kuwarahisishia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam usafiri lakini pia wameona kuna uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.
Kahatano amesema tayari baadhi ya mitandao ya simu imeonyesha utayari wake katika utoaji huduma hizo.
“Tunafanya yote haya ili kuwarahisishia wananchi usafiri na kuwa na chaguo, kwa wale ambao wanataka kupanda usafiri wa hadhi watapanda na wale wenzangu na mimi basi watapanda ule wa daladala.
“Tunataka ifike mahali mtu aache gari lake nyumbani na kupanda usafiri huu ambao pia utachangia kupunguza foleni,” amesema.
Tofauti na daladala, katika usafiri huu, amesema magari yake yatakuwa ni madogo (mini bus) ambapo ndani yake viti vitakuwa vya kuachana kutoka kimoja hadi kingine.
“Kuhusu nauli inategemewa kuwa kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000 lakini zaidi itajulikana zaidi kadri watoa huduma watakavyokubaliana wakati wa ukusanyaji maoni kabla ya kuanza huduma,” amesema Kahatano.
Akielezea namna abiria watakavyopanda vituo tofauti, amesema endapo abiria mmoja atapanda kituo A na mwingine tayari kaomba akiwa kituo B, dereva itamuonyesha kwenye simu yake kwa kumwachia nafasi atakayepanda kituo kinachofuata.
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema, amesema ni jambo zuri kwa kuwa litaongeza wigo wa watu kujiajiri katika sekta ya usafirishaji.
Hata hivyo Lema, amesema anatarajia utoaji wa huduma hizo, hautaathiri ule wa daladala huku akipendekeza walau uwe unatolewa asubuhi watu wanapokwenda kazini au jioni wanaporudi nyumbani.
“Katikati hapo kuanzia saa tano hadi saa nane mchana, hata sisi watu wa daladala tunapata tabu ya kuwapata abiria, sasa wote tukiingia barabarani naona kama itakuwa vurugu, kuwe na ratiba maalumu za watu hawa kutoa huduma hiyo,” amesema Lema.
Baadhi ya wananchi wakitoa maoni yao akiwamo Alice Kimanya mkazi wa Gongo la Mboto, amesema uamuzi huo ni mzuri.
Michael Baregu, mkazi wa Mbagala, amesema huduma hiyo itasaidia kuongeza usalama kwa watumiaji, tofauti na sasa unaweza kupanda gari za watu binafsi kumbe sio watu wazuri na inaweza kutumiwa kama kichaka kwa wahalifu kutekeleza mambo yao.
Minah Imam, mkazi wa Kigamboni, amesema hii itapunguza gharama hasa kwa wale ambao kuna siku anataka atoke na familia.
Usafiri wa kukodi na kulipa Sh3000 unafanywa zaidi katika barabara ya Nyerere ambayo asubuhi huanzia Gongo la Mboto kwenda Mnazi mmoja au Gongo la Mboto-Kariakoo.
Kwa barabara ya Ali Hassan Mwinyi gari hizo zipo zinazotokea Posta kwenda Mwenge mpaka Tegeta na kwa Barabra ya Morogoro, huwa zikianzia Mbezi hadi Kariakoo.