Viongozi wa dini walaani mauaji ya mtoto Amedeus

Rombo. Wakati mwili wa mtoto Amedeus Laurent(7), ukizikwa leo Agosti 13, 2024  nyumbani kwao Kijiji cha Mahango, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, viongozi wa dini na wadau wa haki za binadamu wamelaani mauaji ya watoto yanayoendelea nchini.

Hata hivyo, wanafunzi wa shule alikokuwa akisoma mwanafunzi huyo, wamekuja na  mabango kwenye maziko ya mwenzao yakiwa yameandikwa ujumbe mbalimbali wa kulaani mauaji hayo.

Miongoni mwa mabango yamesomeka, “wazazi pigeni vita ukatili kwa sisi watoto, hata sisi tunayo haki ya kuishi.”

Mwanafunzi huyo wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mawanda, alidaiwa kupotea Agosti 5, 2024 na Agosti 9, 2024  akapatikana akiwa ameuawa kwa kunyongwa.

Inadaiwa kabla ya mtoto huyo kuuawa alilawitiwa na kunyongwa kisha mwili wake kutelekezwa kwenye shamba la mtu ukiwa umefunikwa na majani ya migomba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, akisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa mtupu na kwamba wanamshikilia mtu mmoja kwa kuhusika na tukio hilo.

 “Tunamshikilia mtu mmoja mkazi wa Kijiji cha Mahango wilayani Rombo kwa kumfanyia matendo ya ukatili, udhalilishaji na kumuua kwa kumnyonga mtoto  Amedeus Laurent na kuficha mwili wake kwenye shamba la migomba,” alisema Kamanda Maigwa.

Alisema mzazi wa mtoto huyo alifika kituo cha polisi Agosti 6, 2024  kutoa taarifa ya mtoto wake kutoonekana tangu Agosti 5, 2024 na walianza uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na wananchi,  wakafanikiwa kuukuta mwili huo ukiwa umetelekezwa kwenye shamba la migomba.

Akihubiri katika ibada ya mazishi, Paroko wa Parokia ya Mahida, Padri Ewald Kinyaiya amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha jamii inalindwa.

“Suala la kulea na kuhakikisha usalama unakuwepo katika jamii ni letu sote, Serikali tusijiweke pembeni tukasema ni viongozi wa dini hatutaweza wenyewe kama hatutashirikiana,” amesema Padri Kinyaiya.

Naye, Paroko wa Parokia ya Mrao Mashati,  Padri Emanuel Ndekusara amesema matukio kama hayo yanapotokea katika jamii huiachia familia majeraha makubwa.

Akitoa salamu za pole, msaidizi wa masuala ya kisheria, John Mrina amelaani mauaji hayo na kuwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wanamlimda mtoto na pale wanapoona vishairia vya uhalifu watoe taarifa kwenye vyombo husika.

“Tunalaani vikali kitendo cha ukatili alichofanyiwa mtoto huyu, ni ukatili wa kiwango cha juu, hivyo sisi kama wanajamii tupaze sauti zetu dhidi ya matukio haya ya kikatili yanayoendelea katika jamii zetu,” amesema.

Related Posts