Mwanza. Ikiwa imebaki siku moja Ziwa Tanganyika lifunguliwe Agosti 15, 2024, Serikali imewataka wasimamizi wa Ziwa Victoria kuandaa mkakati wa kulifunga.
Ziwa Tanganyika lilifungwa Mei 15, 2024, ili kutoa nafasi kwa ziwa hilo kupumzika na mazao ya uvuvi kuzaliana na kuongezeka ziwani.
Akizungumza leo Jumanne Agosti 13, 2024, kwenye ufunguzi wa kongamano la Ukuzaji viumbe maji linalofanyika jijini Mwanza kwa siku tatu kuanzia leo mpaka Agosti 15, 2024, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexender Mnyeti amesema bila kufanya hivyo kuna uwezekano mkubwa miaka ijayo viumbe maji wakapotea.
“Ziwa Victoria limetumika sana bila kupumzika, tuwaombe watu wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO), sisi huku hatuwezi kusema tufunge ziwa, hapana, ebu lianze kwenye ngazi husika mjadili kutoka ngazi za chini mpaka lifike huku juu, ili tufike mahala tufanye maamuzi ya kufunga hili ziwa kwa sababu tusipofanya hivyo ziwa hili linapoteza kila kitu,” amesema Mnyeti.
“Tumejaribu kupumzisha Ziwa Tanganyika kuanzia Mei 15 mpaka Agosti 15 ya kesho kutwa ambapo tunaenda kufungua. Tuliwatuma wataalamu wakaleta majibu kuwa mazalia ya samaki na dagaa yameongezeka kwa kiwango kikubwa katika Ziwa Tanganyika, kwa hiyo hili lichukuliwe kwa uzito mkubwa na sisi likija kwetu tutalibariki,” ameongeza Mnyeti.
Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO), Mukasa Bukenya amesema wamepokea maagizo hayo huku akitoa tahadhari kuwa kabla ya kutekeleza, mataifa yanayonufaika ya ziwa hilo yanapaswa kukaa chini kufikiria athari zitakazojitokeza sokoni na kwa wanufaika wa ziwa hilo.
“Ni wazo zuri kufunga ziwa lakini kabla ya kufunga kuna mambo ambayo unatakiwa kuyaangalia kwanza. Saa hizi tunauza hawa samaki sokoni, je, baada ya kufunga na kufungua tutaweza kurejesha soko hilo? Kwa sababu pindi tukifunga mataifa mengine yatapata mwanya wa kutumia masoko yetu,” amesema Bukenya.
“Lakini pia watu wanaotegemea ziwa hili tunatakiwa kuwafikiria pindi tukifunga, je, tuna njia mbadala ya kuwasaidia?” ameongeza Bukenya.
Akitoa maoni kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu wa Machifu nchini ambaye pia ni Chifu wa Mkoa wa Mwanza, Aron Mkomangwa, mbali na kuunga mkono hoja hiyo, ameitaka Serikali kuwekeza nguvu kwenye vizimba ili kuongeza uzalishaji wa samaki.
“Kuna haja ya kuongeza vizimba zaidi ili mazao ya uvuvi yawe mengi zaidi na bei ya samaki iwe nafuu itakayoendana na maisha ya Watanzania. Maana siku hizi mtu kula samaki ni shida kwa sababu samaki wamekuwa adimu na bei imekuwa kubwa,” amesema Chifu Mkomangwa.