WAKATI pazia la Ligi ya Championship likifungwa rasmi leo, kiungo mshambuliaji na kinara wa mabao wa Pamba Jiji, Haruna Chanongo huenda akakosa mchezo wa mwisho wa ligi hiyo dhidi ya Mbuni FC kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja.
Chanongo aliyewahi kuwika Simba, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting, ndiye kinara wa mabao wa Pamba akifunga mabao 12 na kuasisti mara tatu akihusika na mabao 15 kati ya 50 ya timu hiyo inayowania nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara baada ya kuisotea kwa miaka zaidi ya 20 tangu iliposhuka mwaka 2000.
Mchango wa nyota huyo umeifanya Pamba iwe timu ya pili ya Championship yenye mabao mengi ikifunga 50 huku ikizidiwa sita tu na vinara Biashara United yenye 56, lakini Daktari wa timu hiyo, Dishon Chacha aliliambia Mwanaspoti, nyota huyo alitonyesha majeraha aliyokuwa nayo ya nyama za paja kwenye mchezo uliopita dhidi ya TMA Stars ambayo Pamba Jiji ilishinda mabao 2-1.
“Alikuwa na majeraha la paja kwa sababu ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu, nyama zikapanuka na kuchanika na si kwamba aliumia katika mchezo huo bali alitonesha majeraha iliyopelekea kushindwa kuendelea na mchezo,” alisema Dk. Chacha na kuongeza;
“Kucheza itategemea na uamuzi wa waalimu kwani majeraha yake ni ya muda mrefu.”
Mbali na Chanongo, wachezaji wengine wawili Ismael Mtamba na Saleh Seif walioumia katika mchezo na TMA Stars kwa sasa wanaendelea vyema na uwezekano wao wa kucheza mchezo ujao ni mkubwa.
Akizungumzia hali ya kikosi kwa jumla meneja wa timu hiyo, Japhary Juma alisema kikosi kipo tayari kwa mechi hiyo ya leo inayopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha utakaoamua hatma ya Pamba kurudi Ligi Kuu ikifuata Ken Gold iliyopanda mapema wiki iliyopita.
Pamba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 64, alama tatu nyuma ya Ken Gold inayomalizana na Polisi Tanzania leo jijini Mbeya, ikihitaji ushindi zaidi kwani ikipoteza mbele ya Mbuni kisha Mbeya Kwanza iliyopo ya tatu na pointi 62 ikishinda dhidi ya Transit Camp, itaipisha ipande daraja na wao kusubiri play-off sambamba na Biashara United iliyopo ya nne na alama zao 59 na inayomalizana na Cosmopolitan.
Mechi nyingine za kufungia msimu wa ligi hiyo ni TMA dhidi ya Copco, Pan Africans na Stand United, FGA Talents itakayoikaribisha Mbeya City na maafande wa Green Warriors itamalizana na vibonde, Ruvu Shooting iliyoshuka daraja mapema kwa kuganda mkiani mwanzo mwisho tangu kuanza kwa Ligi ya Championship.