Mahakama yamshukia DC Songea, yabatilisha amri yake kumnyima mwananchi hati ya kiwanja

Songea.  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, imebatilisha na kufuta amri iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, iliyomwagiza mkurugenzi wa halmashauri kutotoa hati ya umiliki viwanja kwa mwananchi mmoja.

Hata hivyo, katika shauri hilo namba 6134 la mwaka 2024, mwananchi huyo, Khalfan Kigwenembe, alimshtaki mkuu wa wilaya kwa cheo chake kama mjibu maombi wa kwanza, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa pili.

Katika uamuzi wa maombi hayo uliotolewa jana, Jaji James Karayemaha alisema kama mamlaka ya umma, DC alitumia mamlaka yake kupitiliza na kukiuka haki ya asili kwa kutomsikiliza Khalfan.

Katika hati yake ya kiapo, mwananchi huyo alieleza yeye ndiye mmiliki wa viwanja vilivyopimwa namba 3-4, 6-7 na kitalu MM Songea vilivyopo katika Manispaa ya Songea ambavyo aligawiwa na Halmashauri ya Kijiji cha Sinai mwaka 2011.

Hata hivyo, alipoomba kupatiwa hati miliki (title deed) na mkurugenzi wa halmashauri ya Songea akiwa katika mchakato, DC alitoa maagizo ya maandishi kwa mkurugenzi huyo kusimamisha mchakato huo wa hati miliki.

Amri hiyo ilitokana na malalamiko yaliyowasilishwa kwake na familia ya Zuberi Abdulrahman kwamba, kuna mgogoro juu ya umiliki wa viwanja hivyo.

Baada ya kupokea amri hiyo, mkurugenzi alijizuia kutoa hati hiyo kwa hofu ya kupinga amri ya DC na kwamba, mwananchi huyo anaamini DC hana mamlaka hayo na kwa kuwa hawezi kuyakatia rufaa ndiyo maana akafungua shauri hilo.

Katika hukumu hiyo, Jaji amenukuu barua ya DC ya Oktoba 20, 2023 aliyoituma kwa Mkurugenzi wa halmashauri chini ya kichwa cha habari “Yah: Kutotoa hati ya umiliki wa viwanja mtaa wa Mang’ua Sinai kata ya Lilambo” na ikaendelea:

“…ofisi ya mkuu wa wilaya imepokea malalamiko kutoka familia ya Zuberi Abdalarahman Mbambila kuhusu mgogoro wa ardhi uliopo mtaa wa Mang’ula Kata ya Lilambo, Manispaa ya Songea” inaeleza barua hiyo na kuendelea:

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Songea amenielekeza kuwa nikupe taarifa kuwa unatakiwa usitoe hati ya umiliki wa viwanja plot 3-4 block MM Sinai, Plot 6-7 Block MM Sinai na Plot namba 5 Block MM kutokana na mgogoro wa ardhi.

“…Mgogoro huo unahusu familia ya Zuberi Abdalhaman Mbabila na ndugu Khalfan Kigwenembe. Hivyo basi kwa barua hii unatakiwa usitoe hati miliki ya viwanja hivyo hadi mgogoro wa eneo hilo la ekari 10 utakapokwisha.”

Ombi lilivyokumbana na vigingi

Maombi yake hayo ya kutaka amri hiyo ya DC ifutwe, yalikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wajibu maombi ambao ni DC na AG, kupitia kiapo chao cha pamoja kilichoapwa na Wakili wa Serikali aliyetajwa kuwa ni Egidy Mkolwe.

Katika kiapo hicho, wajibu maombi hao walidai mwananchi huyo hakuwa mmiliki halali wa viwanja hivyo kwa kuwa hakuna nyaraka za kisheria alizoziwasilisha kuthibitisha viwanja hivyo vilipimwa kwa kuwa hakukuwa na nyaraka za upimaji.

Hata hivyo, walikiri DC alipokea malalamiko na kuagiza kusimamishwa utoaji wa hati ya umiliki wa viwanja hivyo na kwamba, mkurugenzi hakusitisha mchakato huo wa utoaji wa hati kwa kuwa barua ya DC haikujibiwa.

Wakili Mkolwe aliyekuwa akisaidiana na wakili Ibrahim Kabelwa, alidai maombi ya marejeo yaliyoombwa na mwananchi huyo yanafanyika katika mazingira ambayo kuna uamuzi umefanyika na malalamiko yalipaswa yapelekwe kwa mkurugenzi.

Kwa mujibu wa wakili huyo, kwa kuwa hakuna maamuzi yoyote kutoka kwa mkurugenzi ya kumnyima hati hiyo, mwananchi huyo hana haki ya kuomba marejeo.

Kuhusu barua ya DC ya Oktoba 20, 2023, Mkolwe alidai haikuwa maamuzi ya mwisho na wala hakuna uthibitisho kama mkurugenzi aliifanyia kazi, hivyo maombi ya mwananchi huyo hayana mashiko kwa kuwa hakuna maombi rasmi aliyofanya.

Wakili wa kujitegemea, Eliseus Ndunguru aliyemwakilisha mwananchi huyo, alieleza kuwa ingawa DC ni mamlaka ya umma, hana mamlaka ya kuzuia mtu asipewe hati kwa kuwa mamlaka hayo ni ya kamishina wa ardhi kwa niaba ya Rais.

Ndunguru alisema ingawa mamlaka hayo yanaweza kukaimishwa kwa maofisa walioidhinishwa katika Serikali za mitaa lakini si DC na wala hana mamlaka ya usimamizi (supervisory power), katika utoaji wa hati za kumiliki ardhi.

Alieleza kwa kuwa amri yake haiwezi kukatiwa rufaa, mwananchi huyo hakuwa na njia nyingine zaidi ya kupinga uharamu huo kupitia mahakama.

Hukumu ya Jaji Karayemaha

Katika uamuzi wake, Jaji alianza kwa kueleza kuwa inavyoonekana wakili Mkolwe alishindwa kufahamu maudhui ya kiapo pamoja na hati ya maelezo  ambayo iliwasilishwa na mwananchi huyo mahakamani.

Kwa asili ya malalamiko hayo, Jaji alisema mwananchi huyo alikuwa analalamikia amri ya DC kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri na kwamba ukiyapitia vizuri, hamlalamikii mkurugenzi ambaye ingelazimika naye aunganishwe.

Jaji alisema katika barua yake, DC hakueleza kama angeupeleka mgogoro huo Baraza la Ardhi ambalo linashughulika na migogoro hiyo, wala kuwashauri wafungue shauri la mgogoro wa ardhi katika Baraza la Ardhi na Nyumba Songea.

“Wala hakusema kwamba amejulishwa na baraza juu ya kuwepo kwa mgogoro huo. Pamoja na yote, maelezo hayo yalitakiwa yapelekwe kwa mkurugenzi ambaye anasimamia maofisa wenye mamlaka ya kutoa hati kwa niaba ya Kamishna,” alisema.

Jaji alisema katika hukumu hiyo, ameipitia barua ya DC Songea kwenda kwa mkurugenzi akimwagiza asitoe hati kwa viwanja vilivyotajwa vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.

“Akiwa kama mamlaka ya umma, DC alitumia mamlaka yake kupitiliza na kukiuka kanuni ya haki ya msingi kwa kushindwa kumuita muombaji kusikiliza upande wake, kabla ya kumuamuru mkurugenzi asitoe hati,” alisema Jaji.

Katika mazingira hayo, Jaji alisema maamuzi ya DC kumwamuru mkurugenzi asitoe hati kama inavyoonekana katika barua yake ya Oktoba 20, 2023 yanabatilishwa na kufutwa kwa kuwa yalitoka katika mamlaka isiyohusika na masuala hayo.

Related Posts