Iran yakataa miito ya kujizuwia kulipiza mauaji ya Haniyeh – DW – 14.08.2024

Iran imekataa wito wa mataifa matatu ya Ulaya walioihimiza kujizuwia kufanya mashambulizi yoyote ya kisasi ambayo yatachochea zaidi mzozo wa kikanda, ikiutaja wito huo uliotolewa na viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kama ombi lililopindukia.

Katika tamko lao la pamoja siku ya Jumatatu, viongozi hao waliitaka Iran na washirika wake kuacha kulipa kisasi cha mauaji ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh mjini Tehran mwezi uliopita, ambayo Iran iliyalaumu kwa Israel.

Soma pia: Iran yapuuza wito wa mataifa ya Magharibi kutoishambulia Israel

Iran | Kumbukumbu ya Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Teheran
Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh aliuawa mjini Tehran, alipokwenda kuhudhuria uapisho wa rais mpya wa taifa hilo.Picha: Rouzbeh Fouladi/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Viongozi hao wa Ulaya pia waliunga mkono msukumo wa hivi karibuni kutoka kwa wapatanishi wa Qatar, Misri na Marekani wa kuratibu mazungumzo ya kumaliza vita vya Israel na Hamas. Mazungumzo hayo yanatazamiwa kuanza tena kesho Alhamisi.

Wakati huo huo, viongozi wa dunia wamelaani hatua ya waziri wa usalama wa Israel Itamar Ben Gvir, kufanya maombi katika uwanja wa Msikiti wa Al-Aqsa ambako alijirekodi akisema Wayahudi wataruhusiwa kusali katika eneo hilo, katika hatua inayokinzana na sheria zinazohusu eneo hilo, ambalo ni mmoja ya muhimu zaidi katika Mashariki ya Kati.

Related Posts