MHE. UMMY NDERIANANGA APONGEZWA KUWASAIDIA WATU WENYE ULEMAVU

Na Mwandishi wetu-Kilimanjaro

Baadhi ya Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Kilimanjaro wamemshukuru Mbunge wa Viti Maalum kundi la Watu Wenye Ulemavu na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga kwa moyo wake wa kujitoa kuwahudumia watu wenye ulemavu.

Wakizungumza mara baada ya mkutano wa ndani uliofanyika katika Tarafa ya Vunjo Mashariki, Wilaya Moshi Vijijini ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Mkoa huo wamesema wamekuwa wakipokea misaada ya vifaa saidizi vikiwemo viti mwendo na fimbo nyeupe kwa wasioona kutoka kwa Mbunge huyo vinavyowasaidia kufanya shughuli zao.

Akizungumza baada ya mkutano huo mkazi wa Njiapanda Himo mwenye ulemavu Bi. Flora Ngowi aliipongeza Serikali kwa kuendelea kupaza sauti kukemea vitendo vya baadhi ya watu wanaowaficha watu wenye ulemavu ndani akisema vitendo hivyo huwanyima fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.

“Tunamshukuru Mhe. Ummy kwa kuendelea kutusaidia sisi watu wa Kata ya Njiapanda kwa kutuletea viti mwendo na amekuwa akipiga kelele sana kwa wazazi au walezi wanaowaficha watoto wenye ulemavu kwa sababu ukishafanya vile wanajikana wakati wana vitu vingi na uwezo wa kufanya mambo makubwa,”Alishukuru Bi. Flora.
Pia mkazi wa Tarafa ya Vunjo Mashariki mwenye mtoto mwenye ulemavu Bi. Sabina Mazengo aliishukuru Serikali kwa kuweka miundombinu rafiki inayoweza kutumiwa katika majengo na mahali penye huduma za kijamii kama hospitali, masoko, vituo vya Daladala na shule kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

“Tunaomba uzidi kutupigania kwa sababu watoto tulionao hapa ni wenye mahitaji maalum kabisa hawasikii, hawaongei na hawatembei tunajua kuna shule zao hivyo tunaomba utusaidie waweze kwenda shule kama watoto wengine wapate haki yao ya elimu,”Aliiomba Bi. Sabina
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum kundi la watu wenye ulemavu na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga aliwapongeza kwa kuendelea kuwatunza watoto hao akisema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa fedha za ujenzi wa mabweni 80 Nchi nzima kwa ajili ya watoto wenye ulemavu waweze kusoma katiika mazingira rafiki na salama.

“Mhe. Rais Dkt. Samia anatupenda sana sisi watu wenye ulemavu mwaka 2022 aliahirisha sherehe za uhuru akatujengea mabweni 80 ya watoto wenye ulemavu ili waende shule na kina mama mfanye kazi. Ninaamini hata kama hawa watoto hawawezi kwenda shule wana vipaji hivyo ninaomba mniamini nitashirikiana na viongozi wenzangu kuhakikisha tunapata namna ya kuwasaidia nawashukuru kwa heshima mlionipa,”Alieleza Mhe. Nderiananga.

Aidha Mhe. Nderiananga alikabidhi mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa Masjid Mussa uliopo katika Tarafa ya Hai Mashariki, Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro.

Related Posts