TFF yamrudisha Awesu KMC, Simba yakwepa rungu

Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeamua kuwa kiungo Awesu Awesu kuwa ni mchezaji halali wa KMC hivyo anapaswa kurejea klabuni kwake.

Kiungo huyo alitangazwa kutambulishwa na Simba na alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwepo katika kambi yao ya maandalizi ya msimu ambayo iliwekwa Misri mwezi uliopita.

Kitendo cha kutambulishwa na kuungana na kambi ya Simba, kiliifanya KMC kupeleka malalamiko TFF ikidai mchezaji huyo alirubuniwa na ana mkataba nao halali.

Muda mfupi baada ya ukurasa wa KMC wa Instagram kumkaribisha Awesu, Mwananchi Digital imeona barua ambayo kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya TFF imeiandika ikiitarifu kuhusu uamuzi wa shauri hilo.

“Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao chake cha tarehe 10.08.2024 ilijadili shauri litilowasilishwa na klabu yako kuhusiana na usajili wa mchezaji Awesu Ali Awesu.

“Malalamiko ya klabu yako ni kuwa Simba SC imemrubuni mchezaji Awesu Ali Awesu, na kumtangaza kuwa mchezaji wao katika mitandano yake ya kijamii bila kufuata utaratibu wakati suala lake likiwa bado halijatatuliwa.

“Kamati ilisikiliza pande zote mbili (KMC FC na Simba SC), na kuamua kuwa Awesu Ali Awesu ni mchezaji halali wa KMC FC, na kama Simba SC inamuhitaji mchezaji huyo izungumze na klabu yake.

“Vilevile Kamati haikupata ushahidi wowote kutoka kwa klabu yako kuwa Simba SC ilimrubuni mchezaji Awesu Ali Awesu. Pia Kamati imetoa onyo kwa Simba SC na kusisitiza ifuate taratibu pale inapohitaji kusajili mchezaji,” imefafanua taarifa ya kamati hiyo.

Related Posts