HATIMAYE sakata la mlinzi wa kulia, Israel Mwenda na Simba limemalizika baada ya klabu hiyo kukubali ombi lake la kuomba kuondoka na kujiunga na timu nyingine.
Taarifa ya Klabu ya Simba imebainisha kwamba, beki huyo wa kulia aliyejiunga na timu hiyo Agosti 2021 akitokea KMC, ameruhusiwa na uongozi wa wekundu hao kuondoka baada ya kuomba kufanya hivyo.
Juni 25, 2024, beki huyo alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba hadi mwishoni mwa msimu wa 2025-26, lakini kabla hajaanza kuutumikia mkataba wake huo, akaomba kuondoka.
“Israel alisaini mkataba mpya wa miaka miwili lakini kabla ya kuanza kuutumikia, aliandika barua ya kuondoka kwa madai ya kuwa amepata timu sehemu nyingine, Simba kwa kujali na kuheshimu maslahi ya mchezaji ilimpa sharti la kurejesha fedha zote na tayari amerejesha.
“Klabu inathamini mchango wa Israel katika miaka yote mitatu aliyodumu kikosini na uongozi wa klabu unamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ya soka.”
Wakati Mwenda akiondoka Simba, inaelezwa kwamba amefikia makubaliano ya kujiunga na Singida Black Stars yenye maskani yake mkoani Singida.