Urusi, Ukraine mambo yazidi kuwa mabaya – DW – 14.08.2024

Kampuni inayoendesha mitambo ya umeme nchini Ukraine, Ukrenergo, ilisema kupitia mtandao wa Telegram kwamba kinu cha nishati kwenye mkoa wa kusini mwa nchi hiyo kilishambuliwa asubuhi ya Jumatano (Agosti 14). 

Ndege zisizo rubani za Urusi zilitumika kushambulia kinu chengine kama hicho cha mkoa wa Chernihiv ulioko kaskazini mwa Ukraine usiku wa kuamkia Jumatano na kusababisha kukatwa kwa huduma ya umeme kwa muda, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni ya Ukrenergo.

Soma zaidi: Ukraine yasema inaendelea kusonga mbele ndani ya Urusi

Kwa upande mwengine, kikosi maalum cha jeshi la Urusi, Rosgvardiya, kilisema kimechukuwa hatua za ziada kulinda mtambo wa nyuklia wa Kursk, mkoa ambao umekuwa ukishambulia vibaya na Ukraine kwa siku kadhaa sasa.

Kikosi hicho kilisema kwenye taarifa yake ya Jumatano kwamba kinadhamiria kuweka msisitizo maalum kwenye mtambo huo ili kuzuwia uwezekano wa droni za Ukraine kuuripuwa mtambo huo, na hivyo kusababisha janga kubwa la miyonzi ya nyuklia. 

Urusi yazidi kulemewa

Usiku mzima wa kuamkia Jumatano, jeshi la Ukraine liliendelea na mashambulizi yake ya droni yanayolenga kuhakikisha udhibiti wao kwenye mkoa huo wa Kursk, katika kile Ikulu ya Marekani ilichokiita “njia panda” kwa utawala wa Rais Vladimir Putin. 

Urusi, Ukraine, Kursk
Mwanajeshi wa Ukraine akipachika bendera ya nchi yake katika mji wa Guevo, mkoa wa Kursk nchini Urusi, tarehe 12 Agosti 2024.Picha: Donbas Operativnyi/Telegram/REUTERS

Urusi ilisema imezidunguwa droni 117 za Ukraine ndani ya mkoa huo wa Kursk, na nyengine kadhaa katika mikoa ya Voronezh, Belgorod na Nizhny Novgorod.

Soma zaidi: Ukraine yasema haina nia ya kulikalia eneo la Kursk huko Urusi

Jeshi lilisema limeyadunguwa pia makombora na kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na wanajeshi wa Ukraine kwenye mkoa wa Kursk.

Gavana wa mkoa wa Belgorod, Vyacheslav Gladkov, alisema “hali ni mbaya sana.”

“Hali kwenye mkoa wetu wa Belgorod inaendelea kuwa ngumu na tete sana. Kila siku makombora ya jeshi la Ukraine yanavurumishwa, yakiharibu nyumba na kuuwa na kujeruhi raia. Kwa hivyo, tumeamua kutangaza hali ya hatari kwenye mkoa mzima kuanzia leo ili kuwalinda watu na kuwasaidia walioathirika, huku tukiiomba serikali ya jimbo kutangaza hali ya hatari kwenye jimbo zima.” Alisema gavana huyo.

Ujerumani yamsaka raia wa Ukraine kwa hujuma ya Nord Stream

Hayo yakijiri, waendesha mashitaka nchini Ujerumani walitoa siku ya Jumatano waranti ya kukamatwa raia mmoja wa Ukraine kwa tuhuma za kushiriki hujuma ya mwaka 2022 dhidi ya bomba la kusafirishia gesi kutoka Urusi la Nord Stream

Mripuko kwenye bomba la gesi la Nord Stream 2 mnamo tarehe 28 Septemba 2022.
Mripuko kwenye bomba la gesi la Nord Stream 2 mnamo tarehe 28 Septemba 2022.Picha: Swedish Coast Guard/AP/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha ARD, waranti wa Umoja wa Ulaya uliombwa mwezi Juni wakati anwani ya makaazi ya mtu huyo ilipokuwa nchini Poland, lakini haikufahamika ni kwa sababu gani mamlaka nchini Poland hazikumtia nguvuni mtuhumiwa huyo ambaye sasa anaaminika ameshatoroka. 

Soma zaidi: Urusi yataka majibu kutoka Magharibi kuhusiana na milipuko ya Nord Stream

Waendesha mashitaka wa Ujerumani wanaamini kuwa raia huyo wa Ukraine, kwa jina la Volodymyr Z., ni mmoja wa wazamiaji waliotega mabomu yaliyoyaripuwa mabomba ya kusafirisha gesi ya Nord Stream mwaka 2022.

Waendesha mashitaka hao wamewatambuwa raia wengine wawili wa Ukraine, mwanamme na mwanamke, ambao wanaamini walijifanya wazamiaji kwenye mashambulizi hayo, ingawa hawajaomba waranti wa kuwakamata.

Reuters, AFP
 

Related Posts