Mwanza. Mahakama ya Rufani iliyoketi Jijini Mwanza, imemwachia huru Shigela Masai ambaye mwaka 2021 alihukumiwa adhabu ya kifo kwa kumuua rafiki yake kwa kumlisha sumu, kisha kukata ulimi na nywele na kuzipeleka kwa mganga.
Kulingana na kosa lilivyokuwa, Masai au kwa jina lingine Mhoja Lukubanija alidaiwa kuwa aliweka sumu kwenye kinywaji ambacho rafiki yake Juma Malinganya alikinywa na baada ya kufa, alichukua viungo hivyo ili akatengenezewa dawa ya kuwa tajiri.
Hukumu ya kumwachia huru ilitolewa Agosti 13, 2024 na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye, Ignas Kitusi na Abdul-Hakim Ameir Issa ambao walisema upande wa mashitaka haukuwa umethibitisha kesi hiyo kwa viwango vinavyokubali.
Adhabu ya kifo ilitolewa Machi 25,2021 na Jaji Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita kupitia kesi ya mauaji namba 239 ya 2016, akiegemea ushahidi wa maelezo ya kukiri kosa na ya ungamo aliyoyaandikwa kwa mlinzi wa amani.
Ilidaiwa kuwa Shigela Masai alimuua Lukubanija ambaye alikuwa jirani yake kwa kumwekea sumu katika kinywaji ambacho alikinywa bila kujua, akakata ulimi na nywele na kumpelekea mganga huyo ili amtengenezee dawa hiyo ya utajiri.
Kulingana na mwenendo wa kesi, mashahidi wawili tu wa Jamhuri, walitosha kuthibitisha shitaka la mauaji ya kukusudia mbele ya mahakama na utetezi wa mshtakiwa wa kukana kufanya mauaji hayo haukutikisa ule wa Jamhuri.
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Inspekta Msaidizi wa Polisi Justo ndiye alichukua maelezo ya onyo ya mshitakiwa wakati shahidi wa pili, Hamad Husein aliyekuwa Mtendaji wa Kata ambaye siku hiyo alikuwa ni mlinzi wa amani.
Maelezo ya onyo na ya ungamo kwa mlinzi wa amani yalitolewa kortini kama kielelezo P3 na P4 na ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa katika maelezo hayo, mrufani huyo mkazi wa Mkoa wa Geita, alikiri kufanya mauaji hayo kwa rafiki yake.
Licha ya mshtakiwa wakati huo akiwa mbele ya Jaji Rumanyika kuyakataa maelezo hayo akidai yalipatikana baada ya kuteswa, kesi ndani ya kesi iliyosikilizwa ilitupa hoja hiyo na kuyapokea na kutengeneza msingi wa kesi hiyo.
Utetezi wake kortini ulivyokuwa
Katika utetezi wake wakati kesi hiyo iliposikilizwa na Mahakama Kuu kanda ya Geita, Shigela Masai ambaye upande wa mashitaka ulimbatiza pia jina la Mhoja Lukubanija, aliiambia mahakama kuwa aliteswa sana akiwa mikononi mwa Polisi.
Alijitetea kuwa aliteswa kiasi cha kulazimishwa akubali kwamba jina lake ni Shigela Masai au Mhoja Lukubanija, wakati jina lake halisi ni Sukran Nkara na akakanusha kutoa maelezo ya kukiri kosa kwa mashahidi hao kama walivyoiambia mahakama.
Hata hivyo, baada ya mahakama kupima hoja za upande wa mashitaka na zile za utetezi, waliamini ushahidi wa Jamhuri na kumtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo, ambayo hakuridhika nayo na kuamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Katika usikilizaji wa hoja za rufaa, Masai au Mhoja kama walivyombatiza, aliwakilishwa na wakili Lenin Njau wakati Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alitetewa na wakili wa Serikali, Castuce Ndamugoba aliyeunga mkono rufaa hiyo.
Wakili Njau, alieleza kuwa mahakama ilikosea kuegemea maelezo ya onyo aliyoyaandika Polisi bila kuwepo ushahidi mwingine unaounga mkono kielelezo hicho na maelezo ya ungamo yasingekuwa mbadala wa ushahidi huo huru.
Kwa mujibu wa Wakili Njau, nayo yalipaswa yaungwe mkono na ushahidi mwingine na kutoa msimamo katika kesi mbalimbali zenye mazingira sawa na kesi hiyo, ambazo zilizowahi kuamuliwa.
Wakili huyo alieleza kuwa hata shahidi wa kwanza hakuwa sahihi kutoa ushahidi kwa kuwa maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa aliyoyaandika, hayakuwa yamesomwa wakati wa mchakato kuhamisha kesi Mahakama Kuu.
Njau alisema hata jina lake halikuwepo katika orodha ya majina yaliyosomwa wakati wa mchakato huo unaojulikana kisheria kama committal, na nafuu pekee ya kutibu athari za kisheria ni kuyatupa maelezo hayo na yale ya ungamo.
Wakili Ndamugoba aliyemwakilisha DPP hakupinga hoja za wakili huyo wa utetezi akieleza kuwa shahidi ambaye hakuorodheshwa kwenye ‘committal’ inakuwa ni kinyume cha kifungu 246 (2) cha sheria ya Mwenendo wa mashauri ya jinai (CPA).
Alisema kwa kuwa upande wa mashitaka haukutumia kifungu 289(1) cha CPA kuomba kibali au kutoa notisi ya kuita mashahidi wengine, ni kosa kubwa kisheria kwa kuwa ilimkosesha mshtakiwa usikilizwaji wa kesi yake ulio wa haki.
Wakili huyo mwandamizi alifafanua zaidi kuwa hata shahidi wa pili wa Jamhuri hakuwa sahihi kutoa ushahidi kwa vile jina lake nalo halionekani katika orodha ya mashahidi ambao maelezo yao yalisomwa kwenye committal.
Kutokana na dosari hiyo ya kisheria, wakili huyo aliiomba Mahakama ya Rufani kuyatupa maelezo hayo yaliyopokelewa kama kielelezo kwa vile ushahidi wa nyaraka wote, huwa unapaswa kusomwa mahakamani wakati wa commital.
Katika hukumu yao, majaji walikubaliana na hoja za mawakili hao kuwa ushahidi wa mashahidi hao wawili na vielelezo walivyovitoa na vikapokelewa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi, vinapaswa kuondolewa katika mwenendo wa kesi.
Walisema baada ya kukubali na kuyaondoa maelezo hayo katika mwenendo huo, upande wa mashitaka unabakia lakini ni kama ushahidi ulioganda ambao hauna maana yoyote na hauwezi kuthibitisha chochote dhidi ya mrufani huyo.
Kuhusiana na hoja ya mrufani kuwa aliteswa hadi kukubali jina la ajabu lisilo la kwake, Jaji aliyemuhukumu alishangaa kwa nini mrufani hakuwaonyesha Polisi ni waongo kwa kuwaleta wazazi, cheti cha kuzaliwa, cha ubatizo au cha shule.
Hata hivyo, jopo la majaji walisema msimamo huo wa Jaji haukuwa sahihi kwani alihamisha mzigo wa kuthibitisha kwa mshitakiwa jambo ambalo si sahihi kisheria, kuhamisha mzigo wa kuthibitisha jambo hilo kwa mshitakiwa.
Kwa mtazamo wa majaji hao, kama Jaji angekuwa na subira kabla ya kukataa utetezi wa mrufani, angebaini kuwa katika maelezo ya onyo aliyoyaandika Polisi, jina la Mhoja Lukubanija walilomlazimisha nalo ndio la mganga wa kienyeji.
Kutokana na maelezo hayo, majaji hapo wameridhika kuwa upande wa mashitaka haukuweza kuthibitisha shitaka hilo na kuacha mashaka, hivyo wanakubali rufaa hiyo na kuamuru mrufani aachiliwe huru kutoka gerezani isipokuwa kama anashikiliwa kwa kosa lingine.