Moshi. Mwanafunzi wa kidato cha tano, katika Shule ya Wavulana ya Umbwe, iliyopo Kata ya Umbwe Onana, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Thomas Edward Kogal (19) amefariki dunia wakati akifanya mazoezi shuleni hapo.
Mwanafunzi huyo ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma, anadaiwa kufariki dunia juzi jioni, Agosti 12, 2024.
Mkuu wa shule hiyo, Elirehema Mungaya akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Agosti 13, 2024, amethibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo huku akisema alikuwa uwanjani akifanya mazoezi na wenzake.
“Ni kweli mwanafunzi wetu amefariki jana (juzi) jioni wakati akiwa uwanjani na wenzake wakifanya mazoezi, lakini alikuwa na tatizo la moyo,” amesema mkuu huyo wa shule.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Agosti 14, 2024, amekiri kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo huku akisema taarifa zaidi atazitoa baadaye.
“Ni kweli kumetokea kifo cha mwanafunzi wa Sekondari ya Wavulana Umbwe, naandaa taarifa nitaitoa baadaye,” amesema Kamanda Maigwa.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Umbwe, Danloard Nyimbi amesema mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo tayari akiwa ameshafariki dunia.
“Kweli tuliupokea mwili wa mwanafunzi kutoka Umbwe Sekondari mwenye umri wa miaka 19, aliletwa na wenzake,” amesema Dk Nyimbi.
Amesema wanafunzi waliomfikisha hospitalini hapo walidai kuwa wakati wanafanya mazoezi, mwenzao huyo aliwaambia anajisikia kuchoka na baadaye aliendelea na mazoezi na ghafla alidondoka chini.
“Hawa wenzake wanasema dakika chache kabla ya kufika kituoni walikuwa wanafanya mazoezi, sasa wanasema kuna kamlima kidogo alikuwa anapandisha, wenzake walienda kama mizunguko 10 hivi, yeye alipoenda mzunguko wa kwanza akadai amechoka, wanafunzi wenzake wakamuuliza nini shida akasema huwa anakula pilipili nyingi.”
Dk Nyimbi anasema wenzake hao baada ya kuelezwa hivyo, waliendelea na mazoezi na walipofika mzunguko wa tatu wakati wanashuka mlima pembeni kulikuwa na mti ndipo alidondoka chini na kupoteza fahamu.
“Wamenisimulia walijaribu kumshtua baada ya kuanguka chini, lakini huenda alipata mshituko wa moyo ila mpaka wanamfikisha hapa kituoni alikuwa ameshafariki dunia,” amesema Dk Nyimbi.
Amesema mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi.
Hata hivyo, Mungaya ameiambia Mwananchi Digital kuwa mwili wa mwanafunzi huyo unatarajiwa kusafirishwa kwenda mkoani Kigoma ambako ndiko nyumbani kwao, kesho kwa ajili ya taratibu za mazishi.