Wahitimu mafunzo ya amali wataka fursa miradi ya maendeleo

Unguja. Vijana waliohitimu mafunzo ya amali wameiomba Serikali kuwapa kipaumbele wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, si tu kuonyesha uwezo wao bali kuwasaidia kupunguza changamoto ya ajira.

Hayo yameelezwa Agosti 14, 2024 wakati wa mahafali ya 10 ya Chuo cha Mafunzo ya Amali Mwanakwerekwe.

Jumla ya vijana 215 wametunukiwa vyeti katika fani tofauti za ushonaji, umeme, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(Tehama), uchongaji na elektroniki.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Asma Masoud Habibu amesema wamekuwa wabunifu katika fani hizo na wana uwezo wa kushindana katika soko la ajira, kwa kuwa wamepata ujuzi, hivyo matumaini yao watakuwa sehemu ya kujenga miradi inayotekelezwa.

“Tunaomba waangalie vijana wanaomaliza mafunzo ya amali kupewa kipaumbele katika soko la ajira ili kutoa hamasa na kuwashawishi vijana wengi wajiunge na mafunzo hayo jambo litakalosaidia kukabiliana na changamoto ya ajira,” amesema.

Amesema wapo waliosoma miaka miwili na wengine miaka mitatu, akieleza walianza wakiwa 165 wanawake 85 na wanaume 80 lakini wamehitimu 138, wengine wakishindwa kuhitimu kwa sababu kadhaa, zikiwamo ndoa na kuhama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Mafunzo ya Amali (VTA), Dk Bakari Ali Silima amesema iwapo vijana wakiandaliwa vizuri ni hazina kubwa kwa Taifa.

Hata hivyo, amesema changamoto waliyonayo ni namna ya kuendesha mafunzo hayo kwa kuwa, yanajikita zaidi kwenye vitendo kuliko nadharia, hivyo vinahitajika vitendea kazi vya kila siku.

“Kuna fani haziwezi kwenda kama hazina malighafi, hapo ndipo utaona umuhimu wa kupata fedha kwa wakati, kwani mitalaa haisubiri kama programu inatakiwa kufanyika kwa miezi minne vinatakiwa vipatikane, visipopatikana inakuwa shida kubwa,” amesema.

Amesema wamejipanga kuwafikia vijana wengi ili kuwainua na kuwaondolea changamoto.

Dk Silima amesema wanakusudia kupita kila shule na majumbani kuhamasisha vijana wajiunge na mafunzo ya amali.

Wanatarajia vijana 1,550 mwakani wajiunge na vyuo vitano vya amali vilivyopo Zanzibar kwa muda mrefu, huku kwa mafunzo ya muda mfupi wapate 2,000.

Tayari SMZ imetengeneza mitalaa inayotaka masomo ya amali yanafundishwe sekondari bila kujali mwanafunzi anataka au hataki.

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma aliyekuwa mgeni rasmi, amesema mafunzo ya ufundi ndiyo chanzo cha maendeleo yote kwa kuwa yanachangia kuwa na miundombinu imara, kukua na kuimarika kwa huduma za kijamii.

Amesema bado hakujawa na mfumo mzuri unaoweza kusaidia upatikanaji wa mafundi kwa urahisi, hivyo ipo haja kubwa ya kuundwa vikundi vya ushirika ili wapatikane kirahisi pindi wanapohitajika.

Mgeni amesema huduma zinaweza kupatikana katika viwanda na taasisi lakini kuna nyingine zinahitajika kwenye jamii kwa hiyo inakuwa vigumu kuwapata.

“Kuna fursa nyingi kikubwa ni kujituma na utayari wenu wa kuchangamkia fursa hizo, kujiingiza katika harakati za uzalishaji kwani Serikali imeona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya mikopo,” amesema.

Amewataka vijana wawe tayari lakini kama hawajajipanga hawataweza kupenya kwenye maisha kwa sababu, “hakuna anayeweza kukupa fedha zake kama hauna uhakika wa kuzitumia vizuri.”

Amesema mambo siyo rahisi, akiwapa moyo wa kuwa wavumilivu, wajasiri na wawe na mipango na mikikakati na wanapopata fedha wazitumie katika uzalishaji.

Related Posts