Mawaziri wa mambo ya nje wa Ethiopia na Somalia hawakufanya mazungumzo ya moja kwa moja mjini Ankara, lakini kupitia waziri wa mambo ya nje wa Uturuki.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan aliwaambia waandishi habari kwamba idadi ya masuala yaliyojadiliwa katika duru hiyo ya pili ya mazungumzo iliongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka ya kwanza, na pia kulikuwa na muunganisho wa baadhi ya kanuni kuu.
Fidan ameongeza kuwa hali hiyo inaashiria kuwepo kwa ufanisi na kuongeza kwamba duru ya tatu ya mazungumzo imepangiwa kuanza Septemba 17 kwa lengo la kufikia makubaliano endelevu na yanayofaa kati ya nchi hizo mbili.
Somalia na Ethiopia zafanya mazungumzo nchini Uturuki
Waziri wa mambo ya nje wa Somalia Ahmed Moallim Fiqi Ahmed alithibitisha kupigwa kwa hatua katika mazungumzo hayo na kusema serikali ya Mogadishu ilikuwa inatazamia matokeo kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Sheria ya Bahari.
Ahmed ameongeza kuwa wanapojiandaa kwa duru ya tatu ya mazungumzo, wana matumaini kwamba kasi waliojenga itapelekea kuwepo kwa suluhisho la mwisho. Waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Taye Atske Selassie amesema nchi yake ilitarajia kuendelea kwa ushirikiano ambao hatimaye utasaidia kutatua tofauti za sasa na kudumisha mahusiano ya kawaida.
Msemaji wa Somaliland,ambayo imejitahidi kutambulika kimataifa licha ya kujitawala na kufurahia amani na utulivu tangu kujitangazia uhuru mnamo mwaka 1991, hakujibu mara moja ombi la tamko.
Sababu ya mazungumzo kati ya Somalia na Ethiopia
Matarajio kabla ya duru ya kwanza ya mazungumzo nchini Uturuki mnamo mwezi Julai yalikuwa chini, huku Somalia na Ethiopia zikionekana kuwa na tofauti zisizoweza kusuluhishwa.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Ankara nchini Uturuki yalijaribu kurekebisha mahusiano kati ya mataifa hayo mawili jirani, ambayo uhusiano wao ulivunjika mwezi Januari wakati Ethiopia ilipokodisha kilomita za 20 za mraba ukanda wa pwani kutoka jimbo linalojitangazia uhuru wake la Somaliland kwa kubadilishana na utambuzi wa uhuru wake.
Somalia yamfukuza balozi wa Ethiopia na kufunga ubalozi
Serikali ya Somalia iliyataja makubaliano hayo kuwa haramu na ilijibu kwa kwa kumfukuza balozi wa Ethiopia nchini humo pamoja na kutishia kufurusha maelfu ya wanajeshi wa Ethiopia walioko nchini humo kusaidia kupambana na waasi wenye itikadi kali.
Uturuki ina uhusiano wa karibu na Ethiopia na Somalia, na pia inatoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Somalia pamoja na kutoa msaada wa kimaendeleo kwa kubadilishana na kipaombele katika njia muhimu ya usafirishaji wa meli kimataifa.
Umoja wa Ulaya watia neno mkataba wa Ethiopia na Somaliland
Chanzo cha kidiplomasia nchini Uturuki kimesema kuwa juhudi za nchi hiyo za kutatua mzozo huo zilianza baada ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kufanya ziara nchini humo mwezi Mei na kuiomba kuingilia kati.
afp/ap