KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Abdul Suleiman ‘Sopu’ atakuwa nje kwa takribani wiki mbili hadi tatu baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimamoto kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Nyota huyo amegundulika kupata majeraha hayo wakati wa mchezo huo uliopigwa Julai 12 mwaka huu, wakati Azam ikishinda mabao 4-0, yaliyofungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mcolombia Jhonier Blanco kila mmoja akiweka kambani mawili.
Daktari wa Azam, Mbaruku Mlinga aliliambia Mwanaspoti, Sopu atakuwa nje kwa wiki mbili, japo kiungo Yahya Zayd anakaribia kurejea uwanjani kufuatia mwezi uliopita kufanyiwa upasuaji wa goti.
“Hali ya majeruhi inazidi kuimarika kwani tayari Abdallah Kheri ‘Sebo’ ameanza mazoezi mepesi na wenzake, hivyo kilichobaki ni kwa benchi la ufundi tu, kuamua kumtumia, tunashukuru baadhi yao wanakaribia kupona kabisa.”
Dk Mbaruku aliongeza kwa upande wa Sospeter Bajana aliyefanyiwa upasuaji wa nyonga Mei 17, mwaka huu Afrika Kusini, anaendelea vizuri na ameanza programu mbalimbali za mazoezi, hivyo muda wowote atajumuika na wenzake.
“Matumaini yetu hadi mwishoni mwa mwezi huu, wote waliokuwa majeruhi watakuwa fiti kuipambania timu, wengine wana majeraha madogo tu, lakini hatutaki kuharakisha kuwatumia kwa vile tunataka wapone vizuri.”
Nyota hao watakosa mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya mabingwa mara 22 wa Ligi Kuu Rwanda, APR kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Agosti 18 na ule wa marudiano utakaopigwa Agosti 24.
Mbali na mchezo huo, pia nyota hao wanaweza wakaikosa mechi ya kwanza ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya JKT Tanzania, mechi itakayopigwa Agosti 28, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.