Dar es Salaam. Viongozi wakuu wa Chadema, Tundu Lissu na John Mnyika, wamesimulia namna walivyokumbana na vipigo na kusafirishwa hadi maeneo tofauti kutoka jijini Mbeya kabla ya kufikishwa Dar es Salaam na kuachiwa huru na polisi.
Mwingine aliyekumbwa na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, ambaye ndiye aliyekuwa wa kwanza kukumbana na msukosuko huo.
Wameeleza hayo leo Jumatano, Agosti 14, 2024, makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu ya kile kilichowatokea kuanzia Agosti 11, 2024.
Viongozi hao walikutana na kadhia hiyo baada ya kukamatwa na polisi wakiwa ofisi za Kanda ya Nyasa, Mbeya, walikokwenda kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani Agosti 12, 2024.
Hata hivyo, maadhimisho hayo hayakufanyika baada ya kuzuiliwa na polisi, na zaidi ya viongozi na wanachama wa Chadema 520, pamoja na waandishi wa habari kutiwa nguvuni. Wengi wamekwisha kuachiwa.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Lissu, Mnyika, Sugu, Twaha Mwaipaya, katibu mwenzi wa Bavicha.
Katika maelezo yake mbele ya waandishi wa habari, Lissu amesema baada ya kuzingirwa na askari polisi katika ofisi ya kanda na giza kuingia, ndipo sintofahamu ilipoanza kwa Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Kamishna Awadh Haji, alipowasili na kuamuru wakamatwe.
“Ilikuwa ni unyanyasaji, kwa sababu walimvuta Sugu hadi kumchania fulana yake. Sasa baada ya hapo kipigo kikaanza kwa kutumia marungu ya umeme, watu walipigwa sana, ilikuwa vurugu. Kilichotokea kwangu, RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya- Benjamin Kuzaga), alinitoa nje na kunikabidhi kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa.
“Sasa huku nyuma niliacha kipigo kikiendelea, watu wanapigwa sana, lakini ghafla nilikuja kuondolewa katika gari la RC0 na kuamriwa nipande gari aina ya pick-up ambayo sikuweza kuipanda kwa namna nilivyo, lakini nikajibiwa kama sina mguu nimekuja kutafuta nini hapa,” amesema Lissu.
Lissu ameendelea kusimulia kuwa, kwa vile hakuweza kupanda, askari waliamriwa wambebe na kumtupa katika gari hilo na kuwekwa katika uvungu wa viti vya gari hilo. Amesema baada ya hapo alipelekwa hadi Mkoa wa Songwe katika kituo cha Polisi cha Vwawa.
“Nilipofika niliwekwa mahabusu. Kesho yake saa tisa jioni nilisafirishwa kuletwa Dar es Salaam. Nilifika Dar es Salaam saa 11 alfajiri katika kituo kikuu, nikajaza karatasi ya kujidhamini mwenyewe kisha nikapelekwa moja kwa moja nyumbani kwangu,” amesema Lissu.
Kwa upande wake Mnyika, ambaye wakati anasogea katika kipaza sauti alionekana akitembea kwa kuchechemea, alidai alianza kuvuliwa miwani yake iliyovunjwa na kutupwa chini na Kamishna Awadh, aliyemwambia kwamba viongozi hao wamekuwa wakisumbua.
“Kwa kauli hii ya Haji ilikuwa kama ishara kwa polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia kunipiga. Walinizunguka wakiwa na silaha nzito pamoja na kunishushia kipigo kwa marungu na mabuti. Nilivyoona hali ile, nikahisi hapa nitapata madhara makubwa kama si kifo.
“Kwa hiyo, kujiokoa nikaamua kupiga kelele za ‘mnaniua mnaniua’ kwa sauti kubwa ili watu wasikie. Wakaamua kunibeba na kunitupa katika gari ambapo pembeni yangu alikuwapo Sugu ambaye hakuwa katika hali nzuri baada ya kipigo,” amesimulia Mnyika.
Mnyika asemadai kuwa walipokuwa wakisafirishwa kutoka Mbeya kwenda Njombe na Iringa, walilazwa chali na hawakutakiwa kuinuka kwa jambo lolote. Wakati safari ikiendelea, Sugu alizidiwa na kulia kutokana na maumivu.
“Niliwaambia askari kuwa Sugu hali siyo nzuri, wakaniambia ajikaze safari bado. Nilipofika Makambako nilitenganishwa na Sugu, yeye aliyepelekwa Iringa.
Mnyika amesema polisi wa Mkoa wa Njombe walikuwa tofauti na wa Mbeya ambapo alipoomba msaada wa chai na koti ili kujilinda na baridi kali lililompiga, alisaidiwa.
Vivyo hivyo, hata gari lililomsafirisha kutoka Makambako hadi Dar es Salaam, lilikuwa ni rafiki, tofauti na alilotoka nalo Mbeya.
Juhudi za kumpata Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji, aliyeongoza operesheni hiyo ili azungumzie tuhuma hizo na kuwa Chadema wamepanga kumshtaki yeye binafsi, zinaendelea.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Agosti 13, 2024, kuhusu tuhuma za kuwapiga viongozi hao, Kamanda Haji alizikana huku akisema kuhusu tukio zima la kuzuia kongamano alishazungumzia mbele ya vyombo vya habari Jumatatu Agosti 12, 2024.
“Siwezi kuzungumzia tena tukio hilo, yote nilishayazungumzia jana katika mkutano wangu na waandishi wa habari na kama kuna suala lingine basi wafuate utaratibu katika kuwasilisha,” alisema Kamanda Haji.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.