Singida kufunga usajili na straika

SINGIDA Black Stars iko katika hatua za mwisho  kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji Abdoulaye Yonta Camara kutoka timu ya Milo ya kwao Guinea, likiwa ni pendekezo la kocha Patrick Aussems. 

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeliambia Mwanaspoti kwamba  mabosi wa Singida wanapambana kukamilisha dili hilo kabla ya usajili haujafungwa leo usiku.

“Kama mambo yataenda sawa basi mchezaji huyo atajiunga na Singida kuichezea msimu ujao,” kilisema chanzo.

Nyota huyo ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Guinea msimu uliopita akiwa na Milo FC ambayo aliifungia mabao 21, inaelezwa ametumiwa tiketi ya ndege kuja nchini huku Mwanaspoti likitambua amepewa mkataba wa miaka mitatu.

Hata hivyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema kama kutakuwa na taarifa yoyote ya usajili viongozi wataweka wazi.

Abdoulaye aliyechezea AS Ashanti Golden Boys na Wakriya AC zote za Guinea, anatua ili kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji linaloongozwa na Joseph Guede aliyetokea Yanga.

Licha ya Guede pia kuna Elvis Rupia na Habib Kyombo, lakini Aussems amependekeza kuongezwa mshambuliaji mwingine huku Abdoulaye akiwa ni chaguo la kwanza.

Related Posts